Mahakama ya juu zaidi nchini Kenya, imeamua kuwa rais
mteule Uhuru Kenyatta atasalia kuwa rais mpya wa Kenya baada ya kusema
kuwa uchaguzi ulifanywa kwa njia huru na ya haki.
Uchaguzi wenyewe ulifanyika tarehe nne mwezi
Machi, ambapo hesabu ya kura ilimpa ushindi Kenyatta kwa zaidi ya laki
nane.
Rais wa mahakama hiyo jaji mkuu
Willy Mutunga alisema kuwa mahakama imekubali kwa kauli moja kuwa
uchaguzi ulifanywa kwa njia ya huru na wazi na kuwa Kenyatta na mgombea
mwenza wake walichaguliwa kihalali.
Uamuzi huu una maana kuwa Uhuru Kenyatta ndiye
ataapishwa kama rais mpya wa Kenya tarehe tisa mwezi ujao
Kesi hiyo iliwasilishwa katika mahakama ya juu
zaidi na mpinzani mkuu wa Kenyatta, Raila Odinga baada ya uchaguzi
uliofanyika mapema mwezi huu.
Matokeo rasmi yalionyesha kuwa Uhuru alishinda
uchaguzi kwa kumpiku Raila kwa asilimia 50.07 huku Raila akipata
asilimia 43.28. Matokeo haya yalizuia kufanyika kwa duuru ya pili ya
uchaguzi kwa kura 8,100.
Bwana Odinga aliishutumu tume huru ya uchaguzi
na mipaka kwa kuhujumu matokeo ya uchaguzi ili kumpa ushindi Uhuru
Kenyatta.
Uchaguzi wa urais, wabunge na wajumbe wengine wa
serikali, ulifanyika tarehe nne mwezi Machi, ukiwa wa kwanza tangu
uchaguzi uliokumbwa na ghasia mwaka 2007 na kusababisha vifo vya watu
zaidi ya elfu moja.
Bwana Kenyatta na mgombea mwenza wake ,William
Ruto,wanakabiliwa na kesi katika mahakama ya jinai kwa kuchochea ghasia
za mwaka 2007. Hata hivyo wamekanusha vikali mashtaka.
Mahakama ya juu zaidi inaweza kuthibitisha
ushindi wa Kenyatta au kuubatilisha uamuzi wa wakenya na hivyo kuitisha
uchaguzi mpya.
Vyovyote matokeo yatakavyokuwa kuna wale
watakaoghadhabika mno.
Rais anayeondoka mamlakani, Mwai Kibaki
amewataka wakenya kuwa watulivu na kukubali uamuzi wa mahakama lakini
wengi wanatagemea sana idara ya mahakama ambayo imekuwa na mageuzi
makubwa na ambayo sasa watu watu imani nayo.
Mawakili wa Odinga wanasema kuwa kesi yao
ilihusisha madai ya kuhujumu hesabu ya kura pamoja na matatizo ya
usajili wa wapiga kura na vile vile matatizo ya mitambo ya usajili wa
wapiga kura.
Mnamo Ijumaa mahakama ya juu zaidi ilidurusu
matokeo ya kura katika vituo 22 vya kupigia kura. Na pande zote mbili
zilisema matokeo yalithibitisha misimamo yao.
Kenyatta ameutaja uchaguzi huo kama ishara ya
kukuwa kwa demokrasia Kenya na ulifanywa kwa njia ya amani.
Tume ya uchaguzi, pia imesisitiza kuwa uchaguzi
ulikuwa huru licha ya hitilafu za kimitambo
Wachunguzi wa kimataifa nao walisema kuwa
uchaguzi ulikuwa huru na wa haki na kuwa tume huru ya uchaguzi
uliendesha uchaguzi huo kwa uwazi.
No comments:
Post a Comment