Friday, March 29, 2013

LEO NI IJUMAA KUU

INAPOFIKA saa tisa alasiri, siku kama ya leo, maarufu kama Ijumaa Kuu, katika nyumba za ibada za Kikristo, kimya hutanda, mishumaa huzimwa na kuashiria kuwa ni siku ya majonzi.

 http://www.topnews.in/usa/files/jesus-crucifixion-full.jpg
Ijumaa Kuu ni siku ambayo Wakristo duniani kote hukumbuka mateso aliyoyapata Yesu baada ya kusulubishwa msalabani yapata zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita. Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimeipa thamani siku hii kwa kuitangaza kuwa ya mapunziko.

Siku hii huadhimishwa kwa ibada inayoambatana na kusoma mistari ya Biblia inayoelezea undani wa matukio yaliyosababisha kusulubiwa kwa Yesu Kristo.

Hii ni siku ambayo inatajwa kuwa na maana kubwa katika imani ya Kikristo. Waumini wanaamini kwamba, kusulubiwa na kufa kwa Yesu, kumeleta ukombozi duniani kote. Ijumaa Kuu haithibitishwi tu na vitabu vya dini, bali hata machapisho ya kihistoria, yanathibitisha juu ya kusulubiwa na kufa kwa Yesu.

Huadhimishwa kwa ibada huku zikitawaliwa na mistari na nyimbo za maombolezo ya kufa kwa Yesu. Rangi za vitambaa vipambwavyo kanisani, huwa ni zile zinazoashiria maombolezo. Hufanyika tangu asubuhi na inapofika saa tisa, muda unaosadikiwa kuwa ndipo Yesu alikata roho, makanisa hutawaliwa na kimya kiambatanacho na kuzima mishumaa ndani ya kanisa. Katika muda huo wengi hutafakari namna walivyokombolewa kwa damu ya Yesu.

Makanisa mengi, vikundi mbalimbali kama vile watoto, vijana na wanawake, hutumia siku hiyo kuonesha maigizo ya kusulubiwa na kufa kwake. Majina yanayotumika katika mataifa mbalimbali, yote hushabihiana kwa kuonesha nafasi ya siku hii. Ingawa majina hayo huweza kutofautiana kulingana na lugha itumikayo katika eneo fulani, lakini yote hulenga kuzungumzia nafasi na umuhimu wa Ijumaa Kuu.

Katika lugha ya Kijerumani, siku hii hujulikana kwa jina la Karfreitag linalomaanisha kuwa ni Ijumaa ya Maombolezo. Waisrael wanaiita Big Friday wakimaanisha ni siku kubwa na maalumu. Nchi za Amerika ya Kilatini, Spain, France, Italia, Ufilipino na Ureno wanaiita Ijumaa Takatifu. ‘Sexta-Feira Santa’ ni neno la Kireno lenye kumaanisha Ijumaa Takatifu.

Katika nchi zenye Wakristo wengi, kama vile Ujerumani, Uingereza Canada na New Zealand, hii ni siku ya mapumziko. Nchi nyingi zinazozungumza Kingereza, maduka mengi mitaani hufungwa kwa ajili ya kuadhimisha siku hii. Nchini Canada, benki, ofisi za serikali na shughuli zote za watu binafsi hufungwa siku hiyo.

Katika Jamhuri ya Ireland, ambayo ni nchi ya Kikatoliki, pombe huzuiwa kuuzwa wakati wa Ijumaa Kuu. Karibu sehemu za starehe na migahawa mingi nchini humo hufungwa kwa siku nzima ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku hiyo kuu. Nchini Ujerumani, ni makosa kufanya maonesho na shughuli mbalimbali za starehe kama vile kucheza muziki siku ya Ijumaa Kuu.

Hatua hiyo ambayo huwagusa hata wasio Wakristo, katika mwongo uliopita, iliwahi kuzua upinzani. Nchini Afrika Kusini, Sheria inatamka kufunga ofisi zote za serikali, shule wakati wa Ijumaa Kuu. Baadhi ya maduka hufungwa pia. Kuuza au kununua pombe pia kunakatazwa. Hapa nchini pia siku hii imo katika orodha ya siku zinazotambulika kuwa ni za mapumziko.

Mafundisho yanasema kwamba sambamba na waumini kuhudhuria ibada, Ijumaa Kuu ni siku kuu ambayo haina budi kutumiwa na Wakristo kutubu dhambi. Ni siku inayowakumbusha upendo wa dhati aliouonesha Kristo. Haipaswi kuchukuliwa kuwa siku ya mapumziko marefu pekee bali na wao pia kutafakari namna wanavyoonesha upendo kwa wengine na kuzidisha kufanya mambo yanayompendeza Mungu.

Ziko tamaduni mbalimbali walizojiwekea Wakristo wengi wakati wa Siku ya Ijumaa Kuu. Miongoni mwake, ni ulaji au kutokula aina fulani ya vyakula na kufunga kula. Hata hivyo, Wakristo wengi hawasubiri kufunga wakati wa Kwaresma au Ijumaa Kuu pekee, bali hufanya hivyo siku zote.

Viongozi wa dini wanafundisha kwamba kujinyima ni jambo la msingi na hivyo inatakiwa iwe ni kujinyima kitu fulani lakini wakati huo huo hicho ulichojinyima kitumike kumsaidia mwenye shida. Licha ya baadhi ya watu kufunga siku ya Ijumaa Kuu wapo ambao wamejiwekea utaratibu wa kufunga kila Ijumaa wakati wengine hufunga siku 40 kabla ya Pasaka.

Suala la kufunga linaloambatana na kutenda yaliyo mema, halina muda wala kikomo. Ulaji wa mkate mdogo aina ya keki hususan kwa jamii za Waingereza, pia ni utamaduni mwingine uambatanao na maadhimisho ya Ijumaa Kuu. Vile vile nyama, ni chakula ambacho waumini wengi wa Kikristo huiepuka.

Wakati awali ilizoeleka kwamba waumini wa madhehebu ya Katoliki ndio wenye utamaduni huo, lakini uchunguzi unonesha kwamba wapo waumini katika madhehebu mengine wanaozingatia pia utamaduni huo. Baadhi ya Walutheri katika nchi za Sweden, Scandinavia, Ujerumani na hata hapa nchini pia wanazingatia utamaduni wa kutokula nyama wakati wa Ijumaa Kuu.

Baadhi ya viongozi wa dini husema kwamba suala la kutokula nyama Ijumaa Kuu siyo imani, bali ni utamaduni. Yaani huchukuliwa kama jukumu binafsi lisilomlazimisha mtu. Viongozi wa dini wamekuwa wakifundisha kwamba maadhimisho ya Pasaka yanapaswa kuambatana na tafakuri kuhusu njia bora za kuendeleza amani kwa mtu binafsi na hata nchi kwa ujumla.

Katika kipindi hiki ambacho nchi za Afrika zinakabiliwa na changamoto ya kuimarisha amani na upendo, kwa mfano, Pasaka inaweza kutumika katika kurejesha hali ya kuvumiliana ili kuepuka migogoro ya kisiasa na kijamii.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...