MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa
Assad (pichani) aliyeapishwa juzi na Rais Jakaya Kikwete amekemea tabia
ya wanasiasa na wafanyabiashara kuingilia kazi za kitaaluma, akisema kwa
upande wake hatapenda kuona watu wa makundi hayo wakifanya hivyo na
kusisitiza kuwa, kufanya hivyo ni kosa.
Aliyasema hayo jana mbele ya waandishi wa habari mara baada ya
ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa kila mwaka wa Wahasibu na Wakaguzi (NBAA)
kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), jijini hapa.
Alisema ofisi ya CAG na watendaji wengine watafanya kazi kwa kufuata
maadili ya kazi, huku akiendelea kusisitiza wanasiasa na wafanyabishara
kila mmoja aheshimu taaluma ya ukaguzi wa hesabu za serikali kwa faida
ya nchi.
Alifafanua kuwa iwapo kila mmoja atawajibika katika nafasi yake na
kuaminiana katika shughuli za kila siku, kamwe hakutakuwa na matatizo
yoyote.
‘’Matatizo ya watu binafsi yasichanganywe na shughuli za kila siku za
ofisi ya CAG na wale wenye kufanya siasa na biashara pia wawajibike
katika nafasi zao na ofisi yangu itafanya mambo kwa kufuata Katiba ya
nchi inavyoelekeza, na sio vinginevyo,” alisema Profesa Assad
aliyekabidhiwa mikoba ya Ludovick Utouh aliyestaafu kwa mujibu wa
sheria.
Alitumia fursa hiyo kuwaasa wahasibu na wakaguzi, akisema wanatakiwa
kufanya kazi kwa weledi mkubwa na kiwango cha hali ya juu ili taaluma
yao iweze kuheshimika nchini. Asante
kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, ukitaka kuwa wa kwanza
kupata habari zetu Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya
neno Jambo Tz