TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa imejadili na kutolea maamuzi pamoja na mambo mengine suala la Madiwani wanane waliotangazwa kufukuzwa uanachama na Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera.
Katika maamuzi yake, Kamati Kuu imebatilisha uamuzi uliofanywa na Halmashauri Kuu CCM ya Mkoa wa Kagera Agosti 13, 2013 wa kuwafukuza uanachama Madiwani hao. Hivyo Madiwani hao wanane ni wanachama halali wa CCM.
Kamati Kuu imetoa uamuzi huo, baada ya kubaini kuwa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera haikuzingatia Katiba ya CCM ya 1977 Toleo la 2012 Ibara ya 93 (15). Ibara hiyo inasomeka kuwa moja ya kazi ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa ni:-
“Kumwachisha au kumfukuza uongozi kiongozi yeyote ambaye uteuzi wake wa mwisho unafanywa na Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa, isipokuwa kwa suala la kumvua uanachama au uongozi Diwani lisifanyike hadi Kamati Kuu imearifiwa na kutoa maelekezo”.