Katikati ni Mwalimu Nyerere akiwa na Katibu wa DABA wa enzi hizo, Jackson Kalikumtima kulia na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Jakaya Kikwete kushoto, sasa rais wa Jamhiri ya Muungano Tanzania. Hii ilikuwa Aprili mwaka 1998 Uwanja wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam.
Na Mahmoud Zubeiry, Bukoba
KADI namba moja ya uanachama wa klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam, inadaiwa alipewa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye leo anatimiza miaka 14 tangu kifo chake, Oktoba 14, mwaka 1999.
Wakati Mwalimu Nyerere anafariki dunia, mimi nilikuwa mwandishi mchanga sana- wakati huo nipo kampuni ya Habari Corporation Limited, chini ya wamiliki wake wa awali akina Jenerali Ulimwengu.
Aliyekuwa bosi wangu wakati huo, Kenny Manara, aliyekuwa Mhariri wa gazeti DIMBA alinipa kazi ya kwenda Uwanja wa Taifa, sasa Uhuru ulipowekwa mwili wa marehemu kwa ajili ya kuagwa ili kuandika habari juu ya wanamichezo waliojitokeza kuuaga mwili wa marehemu na kuchukua maoni yao.
Hakika nilijifunza mengi sana kupitia
msiba huo kwa kusikia, kuambiwa na kujionea. Miongoni mwa niliyoambiwa
ni kwamba, Mwalimu Nyerere ndiye alikuwa ana kadi namba moja ya Yanga SC
na kadi namba mbili, alikuwa nayo hayati Abeid Amaan Karume, rais wa
zamani wa Zanzibar.
Sijabahatika kuiona 'leja' ya Yanga
hadi leo tangu nisikie habari hizo, kwa hivyo siwezi kusadiki, lakini
kulingana na historia ya klabu ya Yanga katika harakati za ukombozi wa
taifa letu, siwezi kupinga hilo.
Nashukuru Mungu nikiwa Mwandishi wa Habari, nimewahi kufanya kazi za kuandika habari katika tukio ambalo Mwalimu Nyerere alikuwepo.
Nashukuru Mungu nikiwa Mwandishi wa Habari, nimewahi kufanya kazi za kuandika habari katika tukio ambalo Mwalimu Nyerere alikuwepo.