Saturday, October 12, 2013

STEWART ADAI SIMBA NA YANGA ZINABEBWA NA TFF


Hall1 1eb67
KOCHA Mkuu wa Azam FC, Muingereza Stewart Hall amesema kwamba ni kazi ngumu Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kupata bingwa nje ya Simba na Yanga kwa sababu timu hizo zinapendelewa mno na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).



Akizungumza Hall amesema kwamba timu nyingine nje ya Simba na Yanga SC ili kuwa bingwa inabidi ifanye kazi ngumu sana ambayo kwa sasa yeye na timu yake, Azam FC wanajaribu.
Kwanza amesema ratiba ya Ligi Kuu inapopangwa inakuwa katika mazingira mazuri kwa timu hizo na mazingira magumu kwa timu nyingine ambazo zinaonekana zikitendewa haki zinaweza kuzima ubabe wa timu hizo katika soka ya Tanzania.
Stewart alitoa mfano hadi sasa katika mechi za Ligi Kuu ambazo tayari zimechezwa, Simba na Yanga kila moja imecheza mechi mbili tu ugenini, wakati Azam FC imecheza mechi sita ugenini, jambo ambalo amesema huwezi kulikuta katika ligi nyingine yoyote duniani.

"Ligi lazima iwe ya uwiano sawa wa mechi za nyumbani na ugenini kwa kila timu, lakini hiyo si kwa hapa Tanzania, kuna ratiba maalum kwa ajili ya Simba na Yanga, namna hii usitegemee soka ya nchi hii ikakua,"alisema.
Lakini pia, Stewart amesema wakati timu nyingine zinacheza mechi 13 nyumbani na 13 ugenini, kwa Simba na Yanga wanacheza mechi saba tu ugenini na hakuna sabau ya msingi katika hilo.
"Sisi Azam ni washindani wa Simba na Yanga katika mbio za ubingwa, lakini hatupati nafasi ya kucheza na hizo timu Uwanja wetu wa nyumbani, tunacheza nao ugenini mechi zote. Kwa nini hawaji Chamazi?"alihoji Stewart.
Lakini pia Stewart alihoji juu ya sababu ya Azam, kwenda kucheza na Ruvu Shooting Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, wakati Simba na Yanga wanacheza na timu hiyo mechi zote Uwanja wao wa nyumbani, Taifa, Dar es Salaam.
"Lakini hii si haki, na kwa namna hii unafikiri lini timu nyingine nje ya Simba itakuwa bingwa hapa, ni vigumu sana, lazima TFF wahakikishe haki inatendeka katika Ligi hii,"alisema.
Pamoja na hayo, Stewart amesema malengo ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa timu yake msimu huu yapo pale pale pamoja na ukweli huo wa Simba na Yanga kubebwa na TFF.
"Tumeanza ligi katika mazingira magumu, tumekuwa na majeruhi wengi na bahati mbaya mwanzoni tu, beki wetu tegemeo Aggrey Morris akapewa kadi nyekundu, lakini tunapambana kuhakikisha tunamudu kucheza ligi katika mazingira haya magumu,".
"Na unaweza kuona hatupo mbali na eneo la ubingwa, tupo nafasi ya pili na wakati wowote tunaweza kupanda kileleni, tunajituma sana kama timu na kila mtu binafsi kuhakikisha tunatimiza malengo tuliyojiwekea msimu huu, kutwaa ubingwa,"alisema. Chanzo: binzubeiry

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...