Rais Jakaya Kikwete
*Asema hatawatetea wauza ‘unga’*Ashangazwa na kiwango cha uongo
RAIS Jakaya Kikwete, amesema anashangazwa na kiwango cha uongo cha baadhi ya wanasiasa ambao hakuwataja majina, kuwa wamekuwa wakizusha madai kuwa Rais aliteua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, bila kuongozwa na mapendekezo ya wadau mbalimbali waliopendekeza majina hayo. Alisema bado anaendelea kuamini mchakato wa Katiba mpya utafikia mwisho wake mwaka 2014 na hivyo kuiwezesha Tanzania kufanya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, chini ya Katiba mpya.
Alisema hana tatizo na watu wanaopinga sera za serikali ama hata kumpinga yeye binafsi, bali tatizo lake ni wanasiasa na wanaharakati wanaochochea ghasia, fujo na uvunjifu wa amani.
Rais Kikwete, aliyasema hayo juzi, mjini San Rafael, California, nchini Marekani, wakati alipokutana na kuzungumza na jumuia ya Watanzania waishio katika Jimbo la California.
Katika hotuba yake, ambayo alizungumzia mambo mbalimbali, Rais Kikwete aligusia mjadala wa karibuni bungeni kuhusu mchakato wa Katiba mpya na kusema kuwa alishangazwa na madai kuwa yeye kama Rais, hakuongozwa na mapendekezo ya wadau wakati anateua Tume ya Katiba.