MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa
Morogoro, leo inatarajiwa kuamua iwapo Katibu wa Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu nchini, Shekhe Ponda Issa Ponda, anastahili dhamana au la,
kutokana na kesi inayomkabili.
Shekhe Ponda alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Agosti 19 na kusomewa mashitaka matatu ya uchochezi yanayomkabili.
Upande wa mashitaka ulidai mahakamani hapo kuwa utaleta mashahidi 15 na vielelezo vitatu, ili kuthibitisha mashitaka hayo.
Baadhi ya vielelezo vitakavyotolewa
mahakamani hapo ni pamoja na DVD mbili, kibali kilichotolewa Agosti mosi
cha kongamano la Kiislamu, kutoka kwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Morogoro
(OCD) na Hati ya Hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Kesi hiyo ya jinai namba 128 ya mwaka 2013, iko mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa Morogoro, Richard Kabate.
Shekhe Ponda katika kesi hiyo, anatetewa
na mawakili watatu wakiongozwa na Wakili Juma Nasoro, wakati upande wa
mashitaka, ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Benard Kongola.