Afya za Watanzania ziko shakani
kutokana na kuwapo kwa biashara ya kuingiza samaki kutoka nje ya nchi,
wanaodaiwa kuharibika na kuuzwa katika la Soko la Feri jijini Dar es
Salaam.
Samaki hao kutoka Yemen, Dubai, China
na Japan, wanaoingizwa nchini wakiwa wameganda kwenye barafu, wengi
huharibika muda mfupi baada ya barafu kuyeyuka au baada ya kununuliwa.
Uchunguzi wa gazeti hili umegundua
kuwa samaki hao huletwa nchini kutafutiwa soko baada ya kukaa kwenye
majokofu kwa muda mrefu huko wanakotoka, kiasi cha kuelekea kuharibika.
Ili wasiharibike, samaki hao aina ya
Marckerel hukaangwa hadi wakauke. Uchunguzi zaidi umebaini kuwa wanunuzi
wake wakuu ni wafanyabiashara wa chakula wakiwamo wamiliki wa migahawa
na Mama Lishe wanaofanya shughuli zao katika miji ya Dar es Salaam,
Pwani, Morogoro na Dodoma.
Samaki hao wanauzwa kwa bei ya chini
ambayo ni Sh38,000 kwa boksi lenye uzito wa kilo 15, ikilinganishwa na
wanaovuliwa hapa nchini ambao bei yake ni Sh60,000, kwa uzito huohuo.
Inaelezwa kuwa samaki hao baadhi yake
ni waleambao wamekwisha muda wake wa kutumika katika nchi hizo, hivyo
kuingizwa nchini kutafutiwa soko.
Gazeti hili lilifika katika soko hilo
kwa siku mbili na kushuhudia samaki hao wakiuzwa kwa wingi, huku wauzaji
wakihimizwa wateja wao kuwahi kuwakaanga au kuwaweka kwenye jokofu.