Wakati Serikali imeeleza nia yake ya kuangalia upya utozaji wa kodi ya kila mwezi kwenye laini za simu za mkononi, imeeleza pia mpango wa kufunga mtambo maalumu ili kubaini malalamiko ya kampuni za simu kudaiwa kuiba fedha za watumiaji.
Katika kile kinachoonesha kusikiliza kilio cha wananchi, Serikali imesema inapitia maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wadau ili kuiangalia upya sheria hiyo ya kutoza kodi ya Sh 1,000 kwa kila laini kwa nia ya kuwapunguzia wananchi mzigo huo.
Serikali imetoa kauli hiyo Dar es Salaam jana kupitia kwa Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa walipozungumza na waandishi wa habari.