SERIKALI ya Tanzania imeipa onyo kali nchi ya Rwanda ikiitaka isijaribu kuota ndoto za kuishambulia kijeshi, vinginevyo itajibu mapigo kwa nguvu zote na kuhakikisha kuwa imeichakaza.
Kauli hiyo ya kwanza nzito imetolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Kimataifa kufuatia taarifa ya matamshi makali yanayodaiwa kutolewa na Rais Paul Kagame wa Rwanda, dhidi ya Rais Jakaya Kikwete na kutishia kuishambulia Tanzania.
Akizungumza na Tanzania Daima jana jijini Dar es Salaam, Msemaji wa wizara hiyo, Mkumbwa Ally, alisema ingawa Serikali ya Tanzania hadi sasa inajua haina ugomvi wowote na Rwanda, lakini amekiri kuwapo kwa kile alichokiita ‘kupishana lugha’ kwa Rais Jakaya Kikwete na Paul Kagame.
Mkumbwa alikiri Serikali ya Tanzania kunasa matamshi yanayodaiwa kutolewa na Rais Kagame katika moja ya hotuba zake aliyoitoa Juni 30, nchini kwake wakati akihutubia katika hafla moja ya vijana.