Kutokana
na kifo cha msanii Albert Mangwea ambaye amefariki nchini Afrika ya
Kusini ambako alikwenda kufanya maonyesho, wasanii mbalimbali
wamezungumzia kifo chake.
Ni
dhahiri, Albert Mangwea alikuwa katika kuutangaza muziki wa Tanzania
nje ya nchi na ndiyo uhai wake ulikopotea, Mwandishi wetu Kalunde Jamal
aliongea na baadhi ya wasanii wenzake na maongezi yakawa kama ifuatavyo:
Joseph Haule a.k.a Profesa Jay
Anasema katika hili hakuna jinsi kwa kuwa kila binadamu atayaonja mauti.
“Inaniuma
sana lakini sina cha kufanya kwa kuwa ni kazi ya Mungu na kazi yake
haina makosa, kinachotakiwa ni kumuombea apumzike kwa amani huko
aendako.
Selamani Msindi ‘Afande Sele’
Anasema
anamtambua Ngwea siyo kama msanii bali ni mdogo wake wa karibu na
ameshindwa kujizuia kutoa machozi kuhusiana na kifo hicho.
Anaongeza
kuwa katika kuonyesha ni kwa jinsi gani kijana huyo alikuwa na mapenzi
na watu kwani kwao ni Morogoro lakini alijulikana ni kijana wa Dodoma
almaarufu East Zoo.
Ngwea
kapambana na muziki ukiwa hauna mbele wala nyuma kapambana kuhakikisha
unakuwa bora lakini kwa sasa ndiyo unatambulika baada ya kufanya
jitihada za kila aina kuufanya uwe ulivyo.”
“Sidhani
kama atanitoka kichwani kwangu, naona kama ametutoroka kwa kuwa
hatuhitaji aondoke muda huu lakini hakuna jinsi tutakutana naye siku ya
mwisho na nitamweleza machungu yangu na kwa jinsi gani kifo chake
kimeniumiza,” anasema.
Snura Mushi ‘Snura’
Anasema
anasikitika sana hasa kwa wao ambao ndiyo kwanza wameingia kwenye
muziki na walitaka kujifunza mengi kutoka kwa wasanii wanaofanya vizuri
kama Mangwea, lakini kwa bahati mbaya au nzuri Mungu amechukua kiumbe
chake hakuna cha kufanya kupinga hilo kwani haliwezekani.