Mrisho Khalfan Ngassa.
Na Saleh Ally
KIUNGO mwenye kasi, Mrisho Khalfan Ngassa, amerejea Yanga na kusaini mkataba wa miaka miwili kuichezea tena timu hiyo.
Ngassa alianza kupata umaarufu mkubwa akiwa na Yanga kabla ya kuondoka na kujiunga na Azam FC kwa kitita cha jumla ya Sh milioni 98 na kuweka rekodi mpya ya usajili.
Lakini Ngassa ameamua kusaini tena mkataba wake mpya Yanga wakati akiwa chini ya klabu ya Simba ambao ni watani wakubwa wa Yanga.
Simba na Yanga zinakutana Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa mwisho kufunga msimu, huku Yanga wakiwa wamepania kulipa kisasi cha mabao 5-0.
Mechi hiyo ndiyo itakuwa ya mwisho kwa Ngassa ambaye mkataba wake umesainiwa bila kuwa na tarehe, Championi Jumatano limeshuhudia na lina uhakika asilimia mia.
“Mkataba na Ngassa kila kitu kimekamilika kama unavyoona, hapa tunachosubiri ni kuisha kwa msimu na mara moja atatua na kuanza kazi Jangwani,” alisema mmoja wa viongozi ambao huhusika na masuala ya usajili Yanga.