Ndugu zangu,
Kama alivyowataarifu kaka yangu Nyaroonyo Kichehere, ni kuwa, jana Jumamosi nilikuwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kuanzia saa tano asubuhi ya jana mpaka saa tatu usiku. Ilihusu mahojiano ya Polisi na mimi kuhusiana na sakata la ndugu yetu Absalom Kibanda.
Ukweli sikukamatwa mahali popote, bali niliitwa na Kamishna ( Upelelezi) Advocate Nyombi. Alhamisi nikiwa Iringa, tukakubaliana na kiungwana na Kamishna Nyombi kuwa nifike Makao Makuu hayo ya polisi Jumamosi saa tano. Ikawa hivyo.
Hapo nilipokelewa na Kamishna Nyombi. Baada ya mazungumzo mafupi ndipo akawaita maofisa wengine watano wa Upepelezi kufanya mahojiano nami.
Niliomba niwe na Mwanasheria, nikakubaliwa. Nilimpigia simu kaka yangu Nyaroonyo, naye, kwa vile ni Wakili pia wa Kibanda akanisaidia kuhakikisha napata wakili mwingine. Pamoja na kuwa ilikuwa ni Jumamosi, ndugu yangu Nyaroonyo Kichehere alifanya alivyoweza.
Ndani ya dakika 40 hivi alifika chumba nr 704 ghorofa ya saba akiwa na Wakili Jacquiline Rweyongeza na Legal Officer Dickson Mbonde. Nilimshukuru Kaka Nyaroonyo Kichehere. Na nilimuaga kwa kumwambia; “ Nenda ukaifahamishe jamii juu ya hiki kilichonitokea”.
Nachukua fursa hii pia kuwashukuru kwa dhati kabisa dada yangu Wakili Jacquiline Rweyongeza na kaka Dickson Mbonde kwa kuacha yote ya Jumamosi na kuwa tayari kuwa msaada kwangu.