Korea Kaskazini hii leo imesema inaingia
katika hali ya vita na Korea Kusini, katika muendelezo wa vita vya
maneno dhidi ya utawala mjini Seoul na Washington, baada ya kuwekewa
vikwazo vya kimataifa kufuatia jaribio lake la silaha za nyuklia.
Shirika la habari la Korea Kaskazini KCNA,
limetoa taarifa inayosema kuwa kuanzia sasa, uhusiano wa Kaskazini na
Kusini utaingia katika hali ya vita, na kwamba maswala yote
yanayojitokeza kati ya Kaskazini na Kusini yatashughulikiwa ipasavyo.
Tangu mwanzoni mwa mwezi huu Korea kaskazini
imekuwa ikitishia kila siku kuishambulia Korea kusini pamoja na kambi za
kijeshi za Marekani, baada ya Marekani na Korea Kusini kuanzisha
mazoezi ya kawaida ya kijeshi na imeyaamrisha majeshi yake kukaa kwa
tahadhari.
Korea kaskazini imetoa kitisho kipya
kuishambulia Marekani, baada ya ndege mbili za Marekani chapa B-2 zenye
uwezo wa kubeba makombora ya nyuklia kufanya mazoezi nchini Korea ya
Kusini.