MBUNGE wa Mbeya
Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA) amesema haungi mkono pendekezo la
Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mbeya kutaka kuuita Uwanja wa Ndege wa
Songwe jina la Rais Jakaya Kikwete.
“Siungi
mkono uwanja kuitwa kwa jina la JK, tunataka jina litakaloasisi
uhalisia wa Mbeya nasi tufahamike kimataifa, kamati ya ushauri ya mkoa
chini ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya mjini, Norman Sigala ilikurupuka kuleta
wazo hilo kabla ya kuwasiliana na wabunge,” alisema.
Alisema
hatua hiyo ya Sigala haiwakilishi mawazo ya wananchi bali inawakilisha
mawazo ya mtu aliyeteuliwa na kwamba wao wakiwa wawakilishi wa Mkoa wa
Mbeya kwa ridhaa ya wananchi hawawezi kukubaliana na suala hilo.
Kauli
ya Sugu iliungwa mkono na wabunge wengine wa Mkoa wa Mbeya, ambapo
Mchungaji Lukson Mwanjale wa Mbeya Vijijini (CCM) alisema anasikitishwa
na hatua hiyo ya kuliwasilisha wazo hilo bila ya kuwashirikisha
wabunge.
Alisema wakati wa kikao cha kamati ya ushauri
wabunge wengi hawakuwepo na taarifa hizo walizisikia baada ya kusoma
kwenye vyombo vya habari.
Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo ambaye pia ni mbunge
wa Songwe, aliomba apewe muda wa kutaka kujua sababu zilizoibua wazo
hilo.
Wazo la kuuita Uwanja wa Ndege wa Songwe jina
la Rais Jakaya Kikwete linazidi kupata upinzani ambapo awali chama cha
NCCR-Mageuzi na kile cha PPT Maendeleo kupitia kwa viongozi wa Mkoa wa
Mbeya vilipinga wazo hilo.
:::TANZANIA
DAIMA:::