Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa leo Jumatatu, Machi 26, imemuachia Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania(TSNP), Abdul Nondo kwa dhamana ya Sh. 5 milioni na mali isiyohamishika.
Nondo amepewa dhamana hiyo mbele ya Hakimu mkazi mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, John Mpitanjia anayeendesha kesi hiyo baada ya mtuhumiwa kukamilisha taratibu zote za dhamana.
Wiki iliyopita, Nondo alinyimwa dhamana baada ya upande wa Jamhuri kudai kuwa ni kwa sababu za usalama wake.
Nondo anayesimamiwa kesi yake na wakili Jebra Kambole anatuhumiwa kwa makosa mawili. Kosa la kwanza ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni Machi 7, 2018 akiwa Ubungo na kusambaza kwa kutumia mtandao wa WhatsApp kuwa yupo hatarini.
Shtaka la pili ni kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa umma mjini Mafinga alipokuwa akitoa taarifa katika kituo cha Polisi Mafinga kuwa alitekwa na watu wasiojulikana jijini Dar es Salaam na kupelekwa Kiwanda cha Pareto cha Mafinga. Kesi imeahirishwa hadi Aprili 10, 2018.
No comments:
Post a Comment