Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akisalimia waumini huku akisikilizwa na Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dkt. Alex Malasusa na Mchungaji Chalres Mzinga baada ya Ibada ya Pasaka katika Kanisa la KKKT la Azania Front jijini Dar es salaam Machi 27, 2016 (Picha na maktaba)
"Fumbua Kinywa chako kwa ajili yake aliye bubu; Uwatetee watu wote walioachwa peke yao; Fumbua kinywa chako, uhukumu kwa haki; uwapatie maskini na wahitaji haki yao" (Mithali 31: 8-9)
Tunapoadhimisha sikukuu ya kukumbuka kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo, tunatambua kuwa utume wa Kanisa letu katika taifa letu, unafanyika katikati ya changamoto kadhaa. Kwa kuwa Kanisa ni sehemu ya jamii, linaguswa na changamoto hizo.
Katika kukaa pamoja na kuliombea taifa letu, sisi maaskofu wa KKKT, tumetafakari na kubaini changamoto hizo. Kwa njia ya salaam za Pasaka, tunaleta kwenu changamoto tatu ili ziongeze mzigo wa kuliombea taifa letu na viongozi wake.
1. Jamii na Uchumi:
Kiini cha Utume wetu katika jamii kinatuingiza kwa nia njema katika maisha ya uchumi na mshikamano wa kijamii. Neno la Mungu linatufundisha kuwa "Mwanadamu hawezi kuishi kwa mkate peke yake" (Luka 4:4).
Pia neno la Mungu linatuhakikishia kuwa Bwana wetu Yesu Kristo alikuja ili tuwe na uzima tele (Yohana 10:10). Tunawiwa katika umoja wetu wa ubaba, kuipongeza Serikali yetu kwa jitihada inazofanya kuboresha maisha ya wananchi.
Tumeshuhudia jitihada na nia njema kuhusu uvunaji na umilikaji wa raslimali za nchi kwa manufaa ya taifa zima. Aidha, tunapongeza jitihada za ukusanyaji wa kodi ili kuiwezesha Serikali kugharamia huduma za jamii.
Hata hivyo, bila kukatisha tamaa jitihada hizo, tunawiwa kushauri yafuatayo:
I. Sekta binafsi na mashirika ya dini ni wadau wa maendeleo, si washindani wa serikali katika kuchangia maendeleo ya taifa. Mazingira yasiyo rafiki kuhusu wadau hawa, ni kikwazo kisicholeta mshikamano kati ya serikali na sekta binafsi na mashirika ya dini katika kuleta maendeleo.
Jitihada za makusudi na za mara kwa mara zifanyike kuondoa dhana ya ushindani kati ya serikali na wadau hawa ili kuimarisha mahusiano mema kati ya serikali na sekta binafsi.
II. Ili mfumo wa ukusanyaji wa kodi uwe endelevu; jitihada za kukusanya kodi ziendane na elimu kwa mlipa kodi. Msisitizo wa uzalendo wa kulipa kodi uende sambamba na ustawi wa walipa kodi katika shughuli zao za biashara.
Mivutano isiyo na tija kati ya walipa kodi (wafanya biashara) na mamlaka ya ukusanyaji wa kodi, inastawisha uadui unaopunguza makusanyo ya kodi na kujenga ushawishi wa rushwa. Mfumo wa kodi unaowafilisi wafanya biashara, haulengi kujenga uchumi wa viwanda.
III. Kutokana na ongezeko kubwa la vijana wasio na ajira; jitihada za wazi na za makusudi zifanyike ili msukumo wa uchumi wa viwanda ufikie matumaini yanayoshikika miongoni mwa vijana wasio na ajira.
Sekta binafsi, wawekezaji na wadau wengine, wahakikishiwe usalama wa mitajiyao kisheria. Hili likifanyika ni kichocheo kizuri cha ujenzi wa viwanda.
IV. Uchumi wa viwanda (vidogo na vikubwa) uendane na uwekezaji katika sekta ya kilimo maeneo ya vijijini. Kilimo na ufugaji ndizo sekta zenye wigo mpana wa viwanda vinavyogusa maisha ya watanzania walio wengi.
Utozaji holela wa kodi na ushuru wa mazao unakatisha tamaa wadau wa kilimo. Migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa upande mmoja, na wakulima/wafugaji na wawekezaji kwa upande wa pili, si kivutio cha uwekezaji katika sekta ya kilimo.
2. Maisha ya Siasa:
Kwa umoja wetu katika utume, tunatambua siasa safi na uongozi bora kuwa ni misingi iliyoongoza maisha ya siasa katika taifa letu. Ujio wa vyama vingi mnamo 1992, haukuondoa umuhimu wa misingi hii bali ulipanua matumizi ya demokrasia iliyojengwa katika uhuru wa mawazo.
Taifa ni mkusanyiko wa taasisi na watu mbalimbali, wenye lengo moja lakini kwa njia mbalimbali. Kutokana na wingi huu, taifa letu daima ni juu ya vyama, taasisi na makundi.
Taifa huongozwa na katiba iliyo kiini cha sheria zote. Taifa haliongozwi na Ilani za vyama. Serikali haiongozwi na Ilani za vyama. Serikali huongozwa na Katiba, Sheria, kanuni na mapokeo mema (misingi na tunu za taifa).
Serikali husimamiwa na Bunge huru lililo sauti ya wananchi. Wananchi ndilo chimbuko la madaraka ya Bunge. Bunge halisimamiwi na ilani, chama chochote wala mtu awaye yote. Kwa umoja wetu na kwa nyakati zetu, hivi sasa tunashuhudia matukio yaliyo kinyume na tunu na misingi iliyolilea taifa letu.
Baadhi ya matukio hayo ni:
I. Hofu iliyojengwa katika matukio halisi yakiwamo utekaji, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.
II. Kupungua na hatimaye kutoweka kwa uhuru wa kujieleza, kukusanyika, na kupata habari. Kwa mwenendo huu, kuna hofu kuwa hata uhuru wa kuabudu uko mashakani.
III. Kubanwa na hatimaye kuelekea kupungua kwa uhuru wa Bunge, Mahakama, na Tume ya Uchaguzi. Hatua hii ni pamoja na kudhoofishwa kwa serikali za Mitaa.
IV. Kukosekana kwa mazingira ya haki na uhuru wa kuchagua na kuchaguliwa katika chaguzi mbalimbali. Chaguzi zote zimeghubikwa na ubabe, vurugu, hila, na vitisho.
V. Utekelezaji wa mipango ya maendeleo wenye mwelekeo wa kiitikadi. Hatua hii imeimarisha ubaguzi wa kiitikadi katika taifa letu na kukuza migawanyiko.
VI. Kushamiri kwa chuki mioyoni mwa watu ambalo ni chimbuko la visasi, kukata tamaa, na ushiriki mdogo wa wananchi katika chaguzi na maisha ya siasa.
VII. Udhalilishaji wa kauli njema isemayo "Maendeleo hayana chama". Udhalilishaji huu unafanyika kwa njia ya kutumia fedha nyingi katika chaguzi ndogo zinazotokana na watu wanaobadili vyama ili kuleta maendeleo. Tunajiuliza, kama maendeleo hayana chama, kwa nini mtu anajiuzuru chama fulani, eti kwenda kuleta maendeleo katika chama kingine? Mchezo huu unagharimu fedha nyingi na maisha ya watu wanaokufa, kujeruhiwa na uharibifu wa mali.
Mambo haya ni tishio linalohatarisha umoja na amani ya nchi yetu.
3. Masuala Mtambuka
Kanisa ni alama ya uwepo wa utume wa kuleta na kutunza matumaini katika jamii. Ukimya wa Kanisa katika masuala yanayoigusa jamii ni ukwepaji wa wajibu wake.
Lakini pia sauti ya Kanisa isiyomilikiwa na mtu isipokuwa Mungu tu, ni chachu ya amani na matumaini. Kwa dhamiri safi inayotokana na
utambuzi wa "Wakati wa Mungu"(Kairos) katika taifa letu, tunawiwa kutambua masuala mtambuka yanayogusa maisha ya watu kipekee na kwa njia nyingi na kuyatolea ushauri ufuatao:
I. Kuhitimisha mabadiliko ya mara kwa mara katika mfumo wa elimu nchini ili kuondoa mwanya wa kila mtendaji mkuu wa wizara kuja na sera yake. Elimu ni kitovu cha ustawi wa taifa, kisiwe kinachokonolewa chokonolewa kila wakati. Sekta zote nchini hujenga mafanikio yake katika mafanikio ya mfumo thabiti wa elimu.
II. Uwezeshaji wa vijana kupata mikopo ya elimu ya juu uwe shirikishi na usiokuwa na "ubaguzi" kati ya wanafunzi wa vyuo binafsi na wale wa serikali; sayansi na sanaa; wazazi maskini na wenye nafasi; waliosoma shule binafsi na wale wa shule za serikali, n.k. Kwa kuwa huu ni mkopo, jitihada ziwekwe zaidi katika urejeshaji wa mkopo huo kwa kuzingatia kuwa huu ni mkopo kwa mtoto siyo kwa mzazi.
III. Vyombo vya usimamizi wa sheria na utoaji haki vionekane vinatenda haki sawa kwa watu wote na makundi yote bila kuacha ishara za fadhila au kukomoana.
IV. Wajibu wa serikali kikatiba katika kulinda uhai wa raia wake, uonekane unatekelezwa bila kuacha mwanya wa kuituhumu serikali. Ukiachwa mwanya katika ulinzi wa uhai wa raia, waweza kutumiwa na mamluki kujichukulia sheria mkononi kwa niaba ya serikali.
Damu isiyo na hatia ina madhara kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo. Mpaka sasa tumeshuhudia umwagaji wa damu unaotusuta sisi sote na mamlaka zote. Mungu anatusuta watanzania kama alivyomsuta Kaini: "Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi" (Mwanzo 4:10).
V. Uhai wa mtu una thamani isiyopimika. Ni wajibu usiokwepeka kuulinda na kuutunza uhai kwa vitendo halisi. Endapo uhai umepotea katika mazingira yoyote, uchunguzi huru na wa haki ufanyike na taarifa zitolewe kwa wakati muafaka ili kujenga jamii yenye imani kwa serikali na vyombo vyake.
Matukio ya mauaji ya askari wetu, mauaji ya raia, majaribio ya kuwaua wanasiasa, utekaji, na uteswaji visipochunguzwa na kutolewa taarifa, ni shina la hofu na uchungu katika jamii. Jamii iliyojaa hofu na uchungu, haiwezi kuwa na maendeleo wala kuwa na roho ya uzalendo.
VI. Ili kulipatia taifa letu ufumbuzi wa mambo yote tuliyotaja na kushauri kwa wakati huu na ujao; tunaisihi serikali ya awamu ya tano, kurejea mchakato wa upatikanaji wa KATIBA MPYA ya wananchi, iliyopendekezwa na wananchi kupitia Tume ya Warioba.
Watanzania wengi wanaona na kuamini kuwa KATIBA MPYA ina majibu ya kukidhi
mahitaji ya taifa letu kwa sasa na baadaye. KATIBA MPYA ni zao la utashi wa Watanzania kupitia tume ya Warioba iliyokuwa na uwakilishi mpana wa taifa letu.
VII. Aidha, tunawashauri raia wema, kwa njia za kidemokrasia kupitia majukwaa ya kikatiba yaliyo katika maeneo yao, kudai upatikanaji wa KATIBA MPYA.
Itapendeza ikiwa KATIBA MPYA itapatikana kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Mambo mazuri yanayofanywa na serikali ya awamu
ya tano yatadumu iwapo kuna KATIBA MPYA inayolinda mazuri.
Kiongozi mzalendo si mbadala wa KATIBA MPYA. Tanzania yenye amani na maendeleo ni tunda la itikadi zote, dini zote, makabila yote na makundi yote chini ya KATIBA MPYA.
C. HITIMISHO
Kufufuka kwa Yesu Kristo ni kiini cha Matengenezo ya Kanisa. Kwamba, katikati ya jamii iliyokata tamaa na kutawaliwa na hofu, Kristo alifufuka na kuleta matumainimapya. Kwamba, katikati ya wasiwasi wa Kanisa kupoteza nguvu ya utume wake, Roho Mtakatifu aliongoza Matengenezo ya Kanisa.
Kwa hiyo Matengenezo ni endelevu katika jamii ya watu na taasisi zao. Muasisi wa Matengenezo Dr. Martin Luther yungali analiwajibisha Kanisa kuzingatia utume wake unaoleta matumainimapya kila siku.
Waliobatizwa wote ni wamisionari tunaotumwa na Bwana wetu Yesu Kristo (Yohana 20:21). Imetupasa kuwa nuru na chumvi ya jamii na kuwa mawakala wa uhuru, umoja na amani.
Taifa letu lilipata uhuru mwaka 1961 bila kumwaga damu. Roho ile ile ya
majadiliano na maridhiano iliyokuwamo ndani ya waasisi wa taifa letu, inatakiwa
kila wakati. Uhuru ulioletwa kwa majadiliano, utunzwe na kulindwa bila ulazima wa kumwaga damu ya watanzania. Uhuru na Umoja ndizo ngao zetu zilizolitunza taifa kwa zaidi ya miaka 50.
Sisi tulio maaskofu kwa neema ya Mungu, tunaleta wito kwenu wenye imani katika dini mbalimbali, kuliombea taifa letu. Kuwaombea wote wenye madaraka ili wajaliwe hekima, busara na upendo kwa taifa na watu wake.
Kupitia jumuia ndogo ndogo na sharika zote, waombee viongozi wetu ili Mungu awajalie na kuwatunuku kiu ya kutenda haki, kusikiliza kuliko kusema, kuelekeza kuliko kuamrisha, kuunganisha kuliko kutawanya, kupenda watu kuliko kutamani kupendwa na watu, kutamani kutumika kuliko kutumikiwa (Marko 10:45), kuheshimu kuliko kuheshimiwa.
Ujumbe wa Pasaka unatuhimiza kuthamini uhai. Bwana wetu Yesu Kristo alikubali kufa ili kuhifadhi uhai wetu. Kwa kufa kwake na kufufuka, amekomesha kifo na mawakala wake. Tunaitwa kuthamini uhai na kutoruhusu tena watu kuteswa na kuuawa.
Kwa hekima yote na unyenyekevu, tunasihi tena, kwamba ikubalike kuwa hitaji la watanzania walio wengi kwa sasa ni KATIBA MPYA. Katiba Mpya ipatikane ili kukuza na kuimarisha mfumo wa utawala utakaolinda uhai wa watu, raslimali za nchi, tunu za taifa, uhuru wa mihimili ya dola, na uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi.
Tunawatakia Pasaka njema ya mwaka 2018, na Mungu awabarikini nyote.
No comments:
Post a Comment