Thursday, July 20, 2017

RAIS MAGUFULI ATOA SIKU 14 VITUO VYA MAFUTA KUFUNGA MASHINE ZA KIELEKRONIKI


Wamiliki wa vituo vyote vya mafuta nchini Tanzania wamepewa siku 14 kufunga na kuanza kutumia mashine za kielektroniki za kutolea risiti la sivyo wafutiwe leseni.

Rais Magufuli, ambaye ametoa agizo hilo, ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhakikisha vituo vyote vya mafuta nchini vinatumia mashine hizo ambazo kwa Kiingereza zinafahamika kama Electronic Fiscal Petrol Printer na kusisitiza kuwa wamiliki watakaokiuka agizo hilo vituo vyao vifungwe na kufutiwa leseni.

"Na kwa hili natoa siku 14, wale wenye vituo vya mafuta wote, uwe upo Chato, uwe Biharamulo, uwe Kagera, uwe Dar es Salaam hakikisha una hiyo mashine, ndani ya siku 14," amesema Dkt Magufuli.

Mwishoni mwa wiki Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) ilivifungia vituo vya mafuta kutokana kutotimiza vigezo baada ya kutofunga mashine za kielektroniki kwenye pampu za mafuta.


Kufikia Jumatatu, vituo vipatavyo 241 nchini humo vilikuwa vimefungwa na kusababisha tatizo la upatikanaji wa mafuta katika miji mingi Tanzania.

Mamlaka ya mapato ilisema wamiliki wa vituo hivyo wamekuwa wakikwepa kulipa kodi kwa kutofunga mashine hizo.

Wakati wa kuanza kutekelezwa kwa agizo hilo Jumapili, vituo 710 vilifungiwa nchi nzima lakini baadaye vituo 469 vikafunguliwa baada ya kulipia mashine hizo kwa mawakala watano walioidhinishwa kufunga mashine hizo kwa vituo vyote takribani 1800 kwa nchi nzima.

Zoezi hilo la kufunga na kutumia mashine hizo lilistahili kuwa limekamilishwa na vituo vyote kufikia Septemba 30 2016 lakini kukawepo na malalamiko toka kwa TAPSOA (Umoja wa wauza mafuta ya petroli na diseli rejareja Tanzania) kuwa mashine hizo zilikua zikiuzwa ghali lakini pia zilikua na shida ya mtandao hivyo zingekwamisha mauzo.

Kwa mujibu wa Tapsoa waliafikiana na TRA kuzitatua changamoto hizo kabla ya kuendelea na zoezi hilo hivyo kuwapa wafanya bishara hao wa mafuta nafasi ya kuendelea na biashara.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...