Monday, March 27, 2017

RIPOTI: FARU JOHN ALIKUFA KWA KUKOSA UANGALIZI WA KARIBU.

Faru maarufu kwa jina John, ambaye alikufa mwaka jana, alikufa akiwa katika hifadhi ya Sasakwa Grumeti kwa kukosa matunzo na uangalizi wa karibu, ripoti ya uchunguzi inasema.

Uchunguzi huo ulioongozwa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele uligundua kuwa kulikuwa na mapungufu katika kumtunza mnyama huyo kabla ya kufa kwake Prof Manyele amesema miongoni mwa mengine, hakukuwepo na kibali rasmi cha kumhamisha Faru John.
Aidha, hakukuwa na mkataba wa kupokelewa kwa Faru John hifadhi ya Sasakwa Grumeti na afya na maendeleo ya Faru John baada ya kuhamishwa haikufuatiliwa. Prof Manyele alisema hayo alipowasilisha ripoti ya uchunguzi kwa Waziri Mkuu wa Kassim Majaliwa.

"Sababu za kifo chake zilichangiwa na kukosa matunzo na uangalizi wa karibu, kukosa matibabu alipoumwa, mazoea yanayotokana na kutofuata taratibu zilizowekwa kisheria na mapungufu ya kiuongozu kwa Wizara husika, hifadhi na taasisi zake," alisema.

Maabara iliyotumika ni ya Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini chini ya usimamizi wa timu ya wataalamu kutoka Tanzania, wachunguzi wa Serikali, chini ya Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Prof Manyele amesema tume yake ilifanya uchunguzi wa kifo cha Faru John kwa kupima vinasaba vya sampuli mbalimbali vikiwemo mzoga, fuvu, mifupa, pembe, damu, ngozi na kinyesi kilichokaushwa ambapo ilibainika kuwa vyote ni vya mnyama mmoja, aina ya faru mweusi ambaye ni dume.

Waziri Mkuu aliiunda tume hiyo Desemba 10, mwaka jana baada ya kupokea pembe mbili za faru John na taarifa yenye nyaraka zilizotumika kumhamisha faru huyo.

Hatua hiyo ilifuatia agizo alolitoa Desemba 6, 2016, akiwa ziarani mkoani Arusha, ambapo alitoa siku mbili na kuutaka uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika kumhamisha faru John kutoka kwenye hifadhi hiyo.

Alitoa agizo hilo alipotembelea ofisi za makao makuu ya NCAA zilizoko wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha na kuzungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...