Wednesday, September 09, 2015

WANAFUNZI 775,729 KUFANYA MTIHANI WA DARASA LA SABA


JUMLA ya watahiniwa 775,729 wanatarajiwa kuanza mtihani wa kumaliza elimu ya msingi utakaofanyika leo na kesho nchi mzima.

Aidha, serikali imesema hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kumzuia mtahiniwa yeyote kufanya mtihani kwa sababu yoyote ile, hata ikiwa ni kutolipa ada.

Akizungumza jana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania, Dk Charles Msonde alisema kati ya hao, watahiniwa wavulana ni 361,502 ambao ni sawa na asilimia 46.6 na wasichana ni 414,227 sawa na asilimia 53.4.

Watahiniwa wasioona walioandikishwa kufanya mtihani ni 76, wakiwemo wavulana 49 na wasichana 27 wakati wale wenye uoni hafifu wanaohitaji maandishi makubwa ni 698, wavulana wakiwa ni 330 na wasichana 368.

“Watahiniwa 748,514 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili na watahiniwa 27,215 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia katika kujifunzia,” alisema.

Msonde alisema katika siku mbili za mtihani, watahiniwa watatahiniwa kwa masomo ya Kiswahili, Kiingereza, Sayansi, Hisabati na Maarifa ya Jamii.

Aidha, Msonde aliwaasa wanafunzi, walimu na wananchi kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu wa mtihani na kuwa Baraza halitasita kumchukulia hatua yeyote atakayeshiriki kwenye udanganifu, ikiwa ni pamoja na kuwafutia matokeo yote watahiniwa watakaobainika kujihusisha na vitendo ya udanganyifu.

Msonde alitoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa na wilaya, kuhakikisha taratibu za mitihani zinazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mazingira ya vituo ni salama, tulivu na kuzuia mianya ya udanganyifu.

Kwa upande wa wasimamizi, Msonde aliwataka kufanya kazi kwa umakini na uadilifu na kujiepusha na vitendo vya udanganyifu, kwani Baraza halitasita kuchukua hatua yoyote dhidi ya atakayebainika kukiuka taratibu za uendeshaji wa mtihani wa Taifa.

Kuhusu kuwazuia watahiniwa kufanya mtihani kwa kisingizio cha kutolipa ada, Msonde alisema mtihani wa darasa la saba ni bure na hauna uhusiano na mwanafunzi kutolipa ada au sababu zingine. “Hakuna mtu yeyote ambaye anaruhusiwa kumzuia mtahiniwa ambaye amejiandikisha kufanya mtihani mwaka huu, hivyo wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanakwenda kwenye vituo vya mitihani,” alisema.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...