Monday, April 20, 2015

LOOO...!!! SIMBA NOMA "INA WAGANGA WENGI WA KIENYEJI KULIKO WATAALAMU WA BENCHI LA UFUNDI"

IMG_9433
Simba waligoma kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo walipocheza na Mbeya City jumamosi iliyopita uwanja wa Sokoine

MTANDAO wa SHAFFIH DAUDA kwa muda mrefu sasa umekuwa ukifanya tafiti na kufuatilia mwenendo wa klabu ya Simba katika mechi za ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu.
Mwishoni mwa juma lililopita, Simba ilifungwa magoli 2-0 na Mbeya City fc katika uwanja wa Sokoine, Mbeya na kuifanya klabu hiyo kongwe nchini kuendelea kukaa nafasi ya tatu kwa pointi 35 walizokusanya baada ya kushuka dimbani mara 22.
Machi 18 mwaka huu walifungwa magoli 2-0 na Mgambo JKT katika uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga, lakini wakashinda 2-1 ugenini dhidi ya Kagera Sugar uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga na ilikuwa aprili 6 mwaka huu (jumatatu ya pasaka).
Katika mechi hizo tatu, mtandao huu ulikuwa unachunguza mwenendo wa Simba na namna wanavyoiandaa timu kwa ajili ya mechi. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Katika mechi ya Tanga waliyochapwa na Mgambo, timu iligoma kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, wachezaji wakakaguliwa ndani ya basi nje ya geti karibu na vyumba vya kubadilishia nguo.
Simba walifanya hivyo wakihofia kurogwa na wenyeji wao, lakini mwisho wa siku wakafa mbili bila na walipoenda Shinyanga kucheza na Kagera walifanya hivyo hivyo, walikataa kuingia vyumbani na kukubali kutozwa faini na TFF.
Simba waliendeleza tabia yao ya kutoingia vyumbani kwa madai ya kuogopa kurogwa huku wakisingizia vyumba ni vibovu. Inawezekana kweli ni vibovu, lakini dhahiri walikuwa na mawazo mengine kichwani mwao kwani viongozi walionekana kuwapangia wachezaji maeneo ya kupita wakati wanaingia uwanjani.

Baada ya safari ndefu ya uchunguzi, hatimaye jibu limepatikana kule Mbeya ambako Simba amekufa tena mbele ya Wagonga nyundo wa Mbeya, Mbeya City fc.
Tulipiga kambi jijini Mbeya na kugundua kuwa Simba wameharibikiwa kwasababu wanawatumia Waganga wa kienyeji kwa muda mwingi wakiamini watawasaidia kupata matokeo ndani ya uwanja.
Dunia ya leo klabu kongwe ya Simba, mfano wa kuigwa inaendekeza imani za kishirikina kwa kiwango cha juu namna hii, inasikitisha sana.
Chakusikitisha zaidi ni kwamba, tunaamini viongozi waliopo madarakani ni vijana wa kidijitali yaani wa kisasa au kileo. Imefika wakati tunaamini wazee kama vile Hassan Dalali na wengineo hizi si zama zao, lakini hayo ni maneno tu, inawezekana wale wazee wakawa na mafanikio makubwa kuliko  vijana ambao tunaamini wanaweza kuiendesha timu kileo au kisasa, vijana ambao ukiwaangalia ni watanashati,  lakini matendo wanayoifanyia klabu ni mabaya mno.
Kwa aina ya viongozi wa sasa wa Simba, ni jambo la aibu kutumia muda mwingi kuwekeza katika uchawi , kutumia waganga au ndumba wakiamini watasaidia kupata matokeo kuliko kujikita katika maandalizi ya kitaalamu na kiuweledi.
Simba wamefungwa na Mbeya City kwasababu hawakutoa nafasi ya kiuweledi katika maandalizi yao, waliwekeza nguvu kwa mambo ya nje ya uwanja wakiamini yatawasaidia kupata matokeo.
Utaratibu ulivyo, unapoenda uwanja wa ugenini, siku moja kabla ya mechi,  timu inatakiwa kufanya mazoezi kwenye uwanja ambao watachezea mchezo, kwahiyo Simba walitakiwa kwenda kufanya mazoezi Sokoine siku ya ijumaa, lakini kutokana na kuamini mambo ya kishirikina hawakwenda kufanya mazoezi siku hiyo, matokeo yake ilibidi wafanye mazoezi kwenye bustani (Garden) ya Hoteli waliyofikia, wanafanyia mazoezi ‘Garden’ eti kwa sababu wanaogopa kurogwa na Mbeya City.
Hii ilikuwa kinyume, mwalimu na benchi la ufundi walitaka timu ikafanye mazoezi uwanjani, lakini baadhi ya viongozi walioandama na timu waliona timu ikienda kufanya mazoezi Sokoine wataenda kupoteza mchezo wa jumamosi.
Mwisho wa siku wakafanya mazoezi uani, wakafanya mazoezi ‘Garden’, na wakawa ‘wamefeli’ rasmi. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Ikaja siku ya mechi, badala ya kupita kwenye mlango wa kawaida wakapitia mlango wa nyuma, wachezaji wakashuka na kuingilia mlango wa nyuma,  wakashindwa kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, wakakaa pembeni kwenye kona kulia kwa jukwaa kuu la Sokoine, sehemu ambayo maaskari Polisi wanapenda kuweka magari yao.
Baadaye kidogo wakaenda karibu na sehemu ya vyumba vya kubadilishia nguo na kukaa nje upande wa kulia kwenye chumba chao , lakini wachezaji wakaamuriwa waondoke tena.
Muda huo wachezaji wa Mbeya City walikuwa wanapasha moto misuli ‘Warm-up) na walikuwa wameshafanya kwa muda mrefu, Simba wao walichelewa hata kupasha moto misuli kutokana na mambo yao ya kishirikina.
Wakati wanaingia kwenye ‘Warm-up’ badala ya kuingilia kwenye benchi ambalo watakaa upande wa kushoto kwasababu kulia walikuwa wamekaa Mbeya City kinyume na taratibu zinazowataka wenyeji kukaa benchi la kushoto na wageni kulia, Simba wakarudi kwenye kona waliyoingilia mara ya kwanza.
Simba walifuata taratibu kwamba wenyeji wanakaa benchi la kushoto, wageni kulia, lakini kulia ni sehemu ambayo Mbeya City wanakaa kila siku na Simba walikataa kukaa kushoto wakiamini pameshapigwa misumari. Walipotaka kukaa kulia Mbeya City wakagoma na ndipo ikatokea vurumai kati ya watu wa Mbeya City na Simba, ikabidi Simba wawe wapole na kukubali kukaa kushoto.
Wakati huo wachezaji walikuwa wamekaa chini nyuma ya lile benchi la ufundi na ilibidi wakafanye ‘warm-up’, kwa itikadi hizo hizo za kishirikiana wakashindwa kuingia uwanjani kupitia eneo hilo, wakaambiwa watembee na kurudi goli la kusini wazunguke kwenye kibendera cha kona na waingie uwanjani na mstari ule wakafanye ‘warm-up’.
Ukiangalia kwa undani,  wachezaji hawataki mambo hayo, wanakasirika, wanaingia uwanjani hawana raha, lakini kwasababu wamelazimishwa na wapambe wanaojifanya wanajua  kila kitu, timu iingilie wapi, wakanyage wapi na kamwe hawataki kukiuka maigizo ya waganda wa kienyeji.
Siku ya mechi hakika wachezaji hawakuwa sawa kisaikolojia, waliingia kupasha misuli na kuanza mechi, wakati wanacheza Mbeya City waliwazidi Simba, walikuwa wamechangamka, walionesha kabisa wanahitaji matokeo, lakini Simba walikuwa wanacheza tu kama vile mtu anayetaka kutekeleza jukumu lake na kuondoka.
Jonas Mkude, Abdi Hassan Banda, Said Ndemla wakawa wanazunguka tu, wanageuka nyuma na mipira, hawaoneshi nia ya kwenda mbele, Elius Maguli, Ibrahim Hajibu wakaonekana vimeo kwasababu walikuwa hawapati huduma kutoka kwa viungo.
Mbeya City walicheza vizuri sana ukiachana na mambo ya kupiga misumari kwa wale wanaoamini hivyo, lakini kwasisi ambao hatuamini hivyo, tukiamini kuwa maandalizi ya mechi ni mazoezi, Mbeya City walicheza zaidi ya Simba, walitengeneza nafasi nyingi na kilichosababisha Simba washindwe kucheza ni imani za kishirikina.
Kuna baadhi ya wachezaji ambao sitaki kuwataja hawafurahishwi na vitendo vya kuendekeza vitendo vya kishirikina, walienda Tanga kuchuana na Mgambo, kuna mtu mmoja wa kamati ya utendaji (jina tunalo) anapenda sana mambo ya kishirikina, alienda na waganga karibia nane (8) Mkwakwani, wakapigwa 2-0 na Mgambo.
Pointi yetu ni kuwakanya Simba na timu nyingine za ligi kuu kuachana na mambo ya kuamini waganga . Hata tabia ya Mbeya City kulinda uwanja, kuchimbua uwanja na kufukia vitu ni ya kishamba, matokeo hayapatikani kwa njia ya Waganda. Mbona kuna mataifa yanasifika kwa uchawi lakini wanaboronga katika soka?
Hata hapa Tanzania maeneo yanayosifika kwa uchawi mfano Sumbawanga mbona hawana hata timu ya ligi kuu?
Inawezekana waganda wanatumika kwasababu ya mila na desturi za kizamani, lakini hayatakiwi kufanyika kwa kasi ya ajabu kama wanavyofanya Simba na timu nyingine.
Kama yanafanyika kwasababu za kitamaduni basi yafanyike kwa siri pasipokuwahusisha wachezaji, haiwezekani eti wamekuja waganga usiku Hotelini, wachezaji wanaamushwa usiku kusikiliza maelekezo ya Waganga.
Unawachosha wachezaji, hawapumuziki vizuri, matokeo yake wanapoteza malengo, inatakiwa mchezaji alale mapema, akae kitandani awaze mechi ya kesho, ajiandae na mechi kisaikolojia, lakini unapomuamsha usiku unamnyima muda wa kupumzika, pia unamnyima nafasi ya kuuwaza mchezo wa kesho na matokeo yake analala na msongo wa mawazo na hasira juu kutokana na kusumbuliwa usiku.
Matokeo yake wanaingia kwenye mechi bila kuwa sawa kisaikolojia na wanafungwa si kwasababu ya kukosa uwezo bali ni miundombinu ya viongozi kushindwa kuwaandaa wachezaji kiuweledi.
Waganga hawasaidii katika soka, maandalizi ya kitaalamu, kiuweledi ndiyo yanatoa nafasi ya kupata matokeo. Simba na timu nyingine zote badilikeni! Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.

Na Shaffih Dauda

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...