Wednesday, January 14, 2015

'HATUFUKUZI MGOMBEA URAIS CCM'

 
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akifungua kikao cha Kamati Kuu ya CCM , mjini Unguja , Zanzibar jana.  Kushoto ni Makamu wake (Zanzibar), Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein .

Wakati Kamati Kuu ya chama tawala, CCM ikimaliza vikao vyake mjini hapa, Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana amesema mambo mengi yanayozungumzwa kuhusu baadhi ya wanachama wanaotajwa kuwania urais hayana ukweli, wala hakuna atakayefukuzwa uanachama.
Kinana aliyasema hayo jana mjini hapa kuhusu mambo yaliyojitokeza kwa wagombea wa nafasi za urais kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu, Oktoba.
Kamati Kuu ya CCM hadi jana jioni ilikuwa ikiendelea na kikao chake kwenye ofisi kuu ya chama, Kisiwandui, Zanzibar.
Kauli ya Kinana imekuja baada ya kuwapo kwa minong’ono kuwa baadhi ya makada waliojitokeza kutangaza ama kuonyesha nia kuutaka urais watachukuliwa hatua, zikiwamo kutimuliwa. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
“Mambo yanayozungumzwa ni mengi kuwa baadhi ya wagombea majina yao yatakatwa. Hayo ni majungu ya kisiasa, yamelenga kuwachokoza viongozi na chama ili wapate cha kusema.
“Chama kina utaratibu na uamuzi unaofanyika kwa vikao maalumu, hizi ni propaganda, ni uchokozi kwa chama chetu,” alisema Kinana.
Wakati Kinana akijaribu kuwaondoa hofu vigogo wanaowania nafasi hiyo, tayari wagombea hao wamepiga kambi mjini hapa, baadhi yao wakiendesha kampeni za chini chini, tangu kumalizika kwa sherehe za Mapinduzi visiwani hapa juzi.
Wagombea hao wamekuwa wakipishana kuingia visiwani na kukutana na baadhi ya wajumbe wa Halmshauri Kuu ya CCM na mkutano mkuu kila upande ukijiimarisha kisiasa kabla ya mchakato wa kumpata mgombea wa urais kupitia chama hicho Mei mwaka huu.
Vikumbo mitaani
Katika hoteli kadhaa mjini hapa baadhi ya makada wamekuwa wakipigana vikumbo ikiwa ni hatua ya kuweka mikakati ya kutengeneza mazingira, hasa ya kukubalika katika chama hicho.
Hata hivyo, tofauti na vikao vingine vya chama hicho tawala, idadi ya wapambe wa makundi yanayotajwa kuwania urais waliofika mjini hapa imekuwa ni ndogo.

Uchunguzi katika baadhi ya hoteli juzi na jana umezishuhudia zikiwa na nafasi, viongozi waliofika kwa ajili ya sherehe za Mapinduzi wakitengewa nafasi kwenye Hoteli ya Serena.
Habari kutoka ndani ya chama hicho, zinasema kuwa makada hao walianza kuwasili mjini hapa siku moja kabla ya sherehe za Mapinduzi na kikubwa kwa baadhi yao, kilikuwa kutafuta kuungwa mkono na wenzao wa Zanzibar.
“Wengine waliondoka jana (juzi) baada ya sherehe. Waliobaki bado wapo katika hoteli wakijaribu kuwasiliana na watu wanaofikiri watawasaidia katika safari yao,” alisema mmoja wa wanachama wa chama hicho.
Mmoja wa wapambe wa mmoja wa makada wanaowania urais, alisikika akizungumza kwa simu katika moja ya mgahawa mjini hapa juzi usiku baada ya kutakiwa na mmoja wa wagombea kutoka Kanda ya Ziwa wakutane.
“Mheshimiwa (akimtaja), uko wapi?, haya nakuja sasa hivi.” alisema na kisha kwenda katika hoteli aliyofikia mgombea huyo.
Makada kadhaa wanatajwa kuwania nafasi hiyo ni pamoja na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Uhusiano na Uratibu) Stephen Wasira, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Fredrick Sumaye.
Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangala, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Tibaijuka akosekana CC
Aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anne Tibaijuka ni mmoja kati ya wajumbe wawili walioshindwa kuhudhuria kikao cha Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya CCM kilichofanyika Kisiwandui. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Mjumbe mwingine ambaye hakuhudhuria ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba.
Akizungumza jana kabla ya kuanza kikao hicho kilichoendeshwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, Kinana alisema wajumbe hao waliomba udhuru.
Hata hivyo, Prof Tibaijuka ni mmoja wa wana CCM waliotajwa kupewa mgawo wa fedha wa Sh1.6 bilioni katika sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
Waziri huyo alivuliwa wadhifa wake na Rais Jakaya Kikwete mwisho wa mwezi uliopita ikiwa ni moja ya utekelezaji wa Maazimio ya Bunge waliyoyatoa mwezi Novemba baada ya kujadili ripoti ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Waziri mwingine ambaye Bunge lilipendekeza avuliwe madaraka, Profesa Sospeter Muhongo wa Nishati na Madini bado anaendelea na wadhifa wake.
Miongoni mwa ajenda zinazotarajiwa kujadiliwa kwenye kikao hicho cha siku moja ni pamoja na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwezi uliopita , hali ya kisiasa nchini na hatima ya wanachama wanaodaiwa kugawiwa fedha hizo.
Utulivu
Tofauti na vikao vingine ambavyo hufanyika Dodoma, mji wa Unguja ulionekana kuwa tulivu bila pitapita za wana CCM waliovalia sare za chama, hata katika maeneo yaliyo karibu na ofisi hiyo, Kisiwandui.
Mapambo yaliyokuwa yakionekana mtaani na katika ofisi za CCM yenye rangi ya kijani na njano, yaliwekwa kama sehemu ya shamrashamra za sherehe za Mapinduzi. Pia, wajumbe wa kikao hicho wengi wao waliokuwa wamevalia sare za chama chao, walionekana wakiingia moja kwa moja katika jengo hilo kuanzia saa 3.00 asubuhi baada ya kusalimiana na wenyeji wao.
Pia, magari na misafara ya viongozi ilifanya maeneo hayo kuwa na ukimya mwingi kama vile hakuna kitu kilichokuwa kinachoendelea kwenye ofisi hizo.
Nje ya ukumbi kulikofanyika kikao, askari polisi na usalama wa Taifa walijipanga kwa mstari karibu na mlango na magari yalikuwa yakiwashusha viongozi mbalimbali.
Hadi saa 11.30 jioni jana, wajumbe walikuwa hawajatoka kwa ajili ya chakula cha mchana au kupumzika.
Hata hvyo, wajumbe wa kamati hiyo walimaliza kikao chao baadaye usiku na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema kuwa suala kubwa lililozungumzwa ni kashfa ya Escrow, hali ya kisiasa nchini na maadili.
“Nitazungumza zaidi kesho (leo) kwa kirefu, kwa kifupi tumezungumzia hayo kwa leo,” alisema Nape akiondoka Kisiwandui.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya kikao hicho, kilipasha kuwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, kimsingi amekubali kufanya uamuzi kuhusiana na masuala mbalimbali ikiwemo la Escrow kabla ya kuanza kwa kikao cha Bunge mjini Dodoma Januari 27.
Kikao hicho cha CC ni cha kwanza kufanyika mwaka huu ambao Tanzania itachagua rais, wabunge na madiwani katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba. Tayari makada kadhaa wametajwa kuwania nafasi hiyo ambapo mwaka jana chama hicho kiliwaadhibu baadhi yao kwa madai ya kufanya kampeni kabla ya wakati. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...