Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za mitaa (LAAC) za Mitaa, Kangi Lugola akizungumza wakati wa kikao cha kamati hiyo kilichofanyika Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mjumbe mwenzake, Omari Nundu.
Licha ya Bunge
kuazimia kuwa wenyeviti wa kamati zake waliotajwa kuhusika kwenye kashfa
ya Akaunti ya Tegeta Escrow wavuliwe nyadhifa zao, hali imekuwa tofauti
katika vikao vya kamati hizo vilivyoanza jana baada ya baadhi yao
kuongoza vikao hivyo. Jana, Kamati Kuu ya CCM imeamua viongozi hao,
Andrew Chenge, William Ngeleja Na Profesa Anna Tibaijuka wafikishwe
Kamati ya Maadili ya chama.
Awali, walitakiwa kuachia ngazi na kamati zao
katika mabano ni Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala), Chenge (Bajeti) na
Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini).
Kikao cha 16 na 17 cha Bunge kiliazimia kuwa
kamati husika za kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka na kwa
vyovyote vile kabla ya Mkutano wa 18 wa Bunge unaoanza Januari 27,
kuwavua nyadhifa zao wenyeviti tajwa wa kamati husika.
Hata hivyo, jana, Ngeleja alisema anaendelea na madaraka yake, kwa kuwa hatua iliyopo sasa ni ya uchunguzi. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
“Mimi naendelea na kazi zangu kama mwenyekiti wa
kamati, najua uchunguzi wa suala hili bado unaendelea, baada ya hapo
ikithibitika ndipo Bunge litachukua uamuzi nami sitakuwa na budi
kutekeleza,” alisema Ngeleja.
Aliongeza: “Ingawa ninajua kuna shinikizo kwa baadhi ya watu kwa sababu wanazozijua wao hawapendi kutuona katika nafasi hizi.”
Kwa upande wake, Chenge alisema: “Sikuwahi
kutangaza kujiondoa katika nafasi hii ya uenyekiti. Nimeshangaa taarifa
zilizotolewa katika baadhi ya vyombo vya habari.”
Alisema tuhuma zinazomkabili hazimuumizi kichwa
kwa sababu hazina ukweli, “Dhamira hainiumi kwa sababu siwezi kushiriki
kuiba fedha za wananchi. Mimi ni kama tumbili hata hapa nitaruka.”
Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Festus Limbu
alisema suala la Chenge linasubiri uamuzi utakaotolewa na Spika wa
Bunge, Anne Makinda. “Kamati imeamua kwa busara Chenge akae pembeni na
makamu mwenyekiti aongoze vikao huku ikisubiri hatua atakazozichukua
Spika (Makinda)...lakini siyo taarifa kwamba Chenge kajiuzulu, siyo
kweli.”
“Unajua suala hili unaweza kusema bado ni bichi,
Chenge ni mwenyekiti mteule wa Spika, lakini wenyeviti wengine
wanachaguliwa na wajumbe wa kamati zao, labda Spika hajaona wa kumteua
au anataka kuiachia kamati ifanye uchaguzi, hili litategemea na yeye,”
alisema Limbu ambaye ni Mbunge wa Magu (CCM)
Kuhusu wafadhili wa maendeleo ambao kamati hiyo
ilikutana nao jana alisema wametoa asilimia 50 ya Dola 558 milioni
ambazo wahisani hao waliahidi.
Kikao cha Kamati ya Nishati na Madini kiliongozwa
na Makamu mwenyekiti wake, Jerome Bwanausi ambaye alilithibitishia
gazeti hili kwamba hawakufanya uchaguzi wowote.
Na Mwananchi
Alipotafutwa kwa simu Mwabalaswa na kutakiwa kuzungumzia hatima yake, alijibu kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo kwenye simu.
Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge, John
Joel alisema: “Suala halipo kikanuni, bali ni maagizo yaliyotolewa na
Bunge kwa hiyo mwenye nafasi nzuri ya kulizungumzia ni Spika.”
Hata hivyo, habari zilizopatikana jana usiku ndani
ya Kamati Kuu ya CCM zilieleza kuwa, Ngeleja, Chenge pamoja na Profesa
Tibaijuka suala lao imeachiwa Kamati ya Maadili ya CCM chini ya
mwenyekiti wake, Philip Mangula.
LAAC yalishukia jiji
Katika hatua nyingine, Kamati ya Bunge ya Hesabu
za Serikali za Mitaa (LAAC), imeitaka Halmashauri ya Jiji la Dar es
Salaam leo itoe taarifa za kueleweka kuhusu uuzaji wa hisa zake na
mikataba kwa Kampuni ya Simon Group. Uamuzi huo umekuja baada ya
Mkurugenzi wa jiji hilo, Wilson Kabwe na Meya, Dk Didas Masaburi
kujichanganya wakati wakijibu maswali ya uuzaji wa hisa hizo kwa kampuni
hiyo ambayo inamiliki Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).
Mwenyekiti wa LAAC, Rajab Mbarouk Mohammed alitoa
maazimio hayo baada ya kuibuka mvutano kati ya wajumbe wa kamati hiyo na
Dk Masaburi na Kabwe kuhusu uuzwaji wa hisa hizo ambazo ni asilimia 21.
Mvutano uliibuka baada ya Mbunge wa Mwibara, Kangi
Lugola kueleza kuwa mmiliki wa Simons Group, Robert Kisena alitaka
kununua hisa hizo, lakini jiji lilikataa.
Kwa upande wake, Kabwe alikiri kuwa walikataa
zisinunuliwe kwa sababu alikuwa na shaka kama Simon Group ingeweza
kulipa fedha zote kama unavyoeleza mkataba. Hisa hizo zinauzwa kwa Sh5
bilioni.
Kitendo cha wajumbe wa kamati hiyo kulichachamalia
zaidi suala hilo ambalo liliwagawa katika Bunge la Bajeti kinatafsiriwa
kuwa ni kutaka kulipa kisasi baada ya Dk Masaburi wakati akitoa
ufafanuzi kuhusu UDA, Mei mwaka jana katika kikao cha Bajeti, kutumia
lugha ya kuudhi kwa wabunge.
Pia, kamati ilihoji kwa nini Jiji la Dar es Salaam
lisivunjwe na kuwa na kitengo kidogo kutokana na kutokuwa na majukumu
ya moja kwa moja kwa wananchi.
Hoja hiyo iliibuliwa na Mbunge wa Msalala (CCM),
Ezekiel Maige kwamba kuna haja ya kuvunjwa kwa jiji hilo na badala yake
kubakiwe watu wachache (meya, mkurugenzi na katibu muhtasi) ambao
watashungulika na masuala mtambuka. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Alisema pia kuna haja ya kuangalia upya, sheria ambayo inaipa
mamlaka halmashauri ya jiji kukusanya ushuru wa maegesho ili kazi hiyo
ifanywe na manispaa za jiji hilo na kisha kutoa gawiwo kwa jiji.
Katika ziara ya LAAC iliyofanya katika manispaa za
jiji hilo hivi karibuni, ilipokea malalamiko ya kutopewa fedha za
maegesho kutoka jiji, jambo linalozikwamisha kufanya shughuli za
maendeleo. Manispaa zote tatu, Ilala, Kinondoni na Temeke zinatakiwa
kugawana asilimia 75 ya mapato ya maegesho na asilimia 25 inabaki jiji.
Akijibu hoja ya ushuru, Dk Masaburi alisema madai
hayo huenda yakawa na ukweli na kuwa tatizo lililopo ni mkataba uliokuwa
umeingiwa na wakala, Nation Park Solution (NPS).
Awali, Mbarouk aliupa uongozi wa jiji siku 19
kuanzia leo kuhakikisha inapeleka ripoti ya tathmini ya mali kwa
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kutokana na
kushindwa kuikamilisha kwa miaka mitatu tangu kutolewa kwa agizo hilo.
PAC yataka uchunguzi NBC
Nayo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC) imemwagiza Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru kuteua
mkaguzi binafsi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa sababu za kushuka kwa
mtaji wa Benki ya NBC ambayo inadaiwa Sh22.5 bilioni na Kampuni ya Absa
Group Limited ya Afrika Kusini.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alitaja maeneo
yaliyosababisha mtaji kushuka kuwa ni mikopo iliyotolewa kwenye sekta ya
usafirishaji, utekelezaji wa sera za Benki mama ya ABCA na mfumo wa
uhasibu uliotambua mapato hewa. Iwapo Serikali itashindwa kulipa deni
hilo hadi Machi mwaka huu, itapoteza asilimia 30 ya hisa zake katika NBC
na hivyo benki hiyo kuwa chini ya Kampuni ya Absa ambayo ina asilimia
55 ya hisa za NBC.
Awali, kampuni hiyo ilikuwa na hisa asilimia 70 za
benki hiyo lakini ikauza asilimia 15 ya hisa zake kwa Shirika la Fedha
la Kimataifa.
Serikali ilikopa kiasi hicho cha fedha ili
kutekeleza agizo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo mwaka 2012
iliiagiza NBC kuongeza mtaji wa biashara wenye thamani ya Sh75 bilioni,
baada ya ule wa awali kushuka kwa asilimia 12.
Baada ya NBC kubinafsishwa mwaka 1997, Serikali
ilibaki na asilimia 30 ya hisa na Kampuni ya Absa kuchukua asilimia 70,
mtaji wa NBC ulishuka kati ya mwaka 2010 hadi 2012 baada ya benki hiyo
kutoa mikopo ya magari wa Sh55 bilioni.
Baada ya mtaji wa NBC kushuka kwa asilimia 12,
Benki Kuu Tanzania (BoT), iliagiza wanahisa wote watatu kuongeza mtaji.
Kwa kuwa Serikali haikuwa na fedha za kuongeza katika mtaji, ilikopa
Sh22.5 bilioni kwa Absa na kuzitoa kama mtaji kwa makubaliano ya
kurejesha deni hilo ndani ya miaka miwili. Kuhusu taasisi ya mikopo ya
Pride, Msajili wa Hazina alisema baada ya ukaguzi wa CAG walibaini kuwa
taasisi hiyo iliondolewa kimakosa katika orodha ya taasisi za umma.
Alisema kutokana na hali hiyo kuna hasara ambayo serikali imeipata na
kusisitiza kuwa watapokea taarifa rasmi ya uchunguzi wa taasisi hiyo
uliofanywa na CAG na wataiwasilisha katika vikao vya Bunge vinavyoanza
Januari 27. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment