Baadhi ya makada wa wa CCM wanaotajwa
kuwania urais kupitia chama hicho wanadaiwa kugeuza mkutano wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec), kuwa sehemu ya kampeni kwa wajumbe wa
mkutano huo wakidaiwa kumwaga fedha usiku kucha.
Gazeti hili lilishuhudia kampeni hizo zikifanywa
na wapambe wa wagombea hao nje ya Ukumbi wa Nec uliopo nje ya jengo la
White House mjini Dodoma na baadhi ya watu wanaotajwa kuwania nafasi
hiyo.
Wapambe hao kwa siku mbili za vikao vya Nec
vilivyofanyika mjini hapa kuanzia juzi walionekana wakifika mapema,
kusalimia, kujitenga katika makundi madogomadogo na wajumbe wa Nec
tofauti na vikao vingine vilivyotangulia.
Harakati hizo hazikuishia katika viwanja hivyo,
bali hata nje ambapo mmoja wa makada anayetajwa kuwania nafasi hiyo
kutoka Kanda ya Ziwa ameonekana kukutana na makatibu wa CCM katika moja
ya hoteli mjini hapa. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
“Huyu jamaa amekutana na makatibu wa CCM mara
nyingi katika kile kinachoelezwa kuwa ni kusaka wajumbe ili wasijiunge
na kambi nyingine,” kilieleza chanzo chetu.
Alipoulizwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,
Nape Nnauye, alisema bado hajazipata taarifa hizo na kwamba kama kuna
vitendo vya rushwa vinafanyika ni nje ya mazingira hayo.
Alisema katika mazingira kunapofanyika kikao cha Nec, si rahisi kuwapo vitendo hivyo.
“Sasa kama wanapeana barabarani mimi itakuwa ni
vigumu sana. Mimi ninashughulikia na mambo ya humu ndani (kikao cha
Nec),”alisema na kuongeza:
“Leteni taarifa nilikuta fulani anagawa ama fulani
anapokea, haya maneno ya jumla hivi yanaweza kuwa ni mkakati wa kupaka
chama matope,” alisema.
Alisema kama inagawiwa usiku wakati yeye akiwa amelala hawezi kufahamu.
Makatibu na wenyeviti wa CCM wa wilaya wanaingia katika Nec kwa mujibu wa vyeo vyao.
Tayari hali hiyo imelalamikiwa na baadhi ya wajumbe wa Nec, wakisema inakitia aibu chama.
Mmoja wa wajumbe wa Nec, Juma Kilimbah, alisema kitendo cha
kufanya kampeni ya kutaka kuungwa mkono ni kinyume cha maadili ya chama.
“Mimi sijafuatwa lakini kama kuna watu wanafanya
kampeni ya kutaka kuungwa mkono wakati chama hakijatangaza kuanza kwa
mchakato ni kinyume cha maadili ya chama,” alisema.
Rushwa hiyo inadaiwa kufanywa na waratibu wa kundi
moja linalomuunga mkono mmoja wa vigogo nchini, ambaye anatajwa kuwania
nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.
Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini
kumekuwa na waratibu kutoka kanda mbalimbali ambao waligawanywa katika
makundi manne na walikuwa wakitoa fedha kwa baadhi ya wajumbe wa Nec ili
wamuunge mkono ‘mgombea’ huyo.
Rushwa hiyo imekuwa ikitolewa kwa usiri mkubwa na
mmoja wa viongozi wa chama hicho ambaye aliwahi kufanya kazi mkoani Dar
es Salaam, anaelezwa kuwajibika katika kuwapeleka wajumbe wa Nec ili
wakalipwe kwa mmoja wa waratibu wa mpango huo ambaye imedaiwa ni mmoja
wa mawaziri. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Kwa mujibu wa chanzo chetu, wajumbe hao walikuwa
wakipewa shilingi milioni moja kama ushawishi ili wamuunge mkono
‘mgombea’ huyo.
Hata hivyo, habari za kutolewa kwa rushwa hizo
zilivuja mara baada ya mmoja wa waratibu wa mpango huo kutoka kanda ya
Nyanda za Juu Kusini kuwapa wajumbe Sh700,000 badala ya shilingi milioni
moja, jambo ambalo liliwachefua wajumbe waliopunjwa mgawo huo.
Wajumbe waliolengwa zaidi ni wale walioonyesha nia
ya kuhamia kwenye kundi la mgombea mwingine, anayeonekana kuwa na nguvu
zaidi ya wenzake.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, kampeni za kutafuta
wajumbe wa Nec wanaowaunga mkono, zinalenga katika mmoja wa watu
wanaotajwa kuwania urais kuwa na uhakika wa kupata kura zaidi 190 kati
ya wajumbe 370 wa Nec.
Akizungumza kwa njia ya simu kuhusu madai hayo,
Mkuu wa Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wa Mkoa
wa Dodoma, Emma Kuhanga, alisema hawajapokea madai yao.
Hata hivyo, aliahidi kufanyia kazi taarifa alizozipata kutoka kwa mwandishi wa habari.
“Hatujapata madai hayo lakini kutokana na swali lako tunalichukulia kama taarifa ya kuanza kufanyia kazi,” alisema.
WanaCCM ambao wamekuwa wakitajwa kuwania urais ni Waziri Mkuu
Mizengo Pinda, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu),
Stephen Wasira, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na mtangulizi wake
katika nafasi hiyo, Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi
Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel
Nchimbi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe.
Wengine ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta. Wengine wanaotajwa ni Waziri wa Uchukuzi, Dk
Harrison Mwakyembe, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose
Migiro.
Pia wamo Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Tayari CCM imeshawafungia kufanya kampeni baadhi ya makada wake walioonekana kuanza kufanya kampeni kabla ya muda.
Waliotangazwa kufungiwa na kuwekwa chini ya uangalizi ni Lowassa, Membe, Makamba, Ngeleja, Wasira na Sumaye. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Na Mwananchi
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment