Wednesday, August 20, 2014

WANAFUNZI BILA KUANDAMANA HAWAPATI HAKI ZAO...???


Sasa ni dhahiri kwamba Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu (Tahliso) imepata mwarobaini wa matatizo yake, ikiwa ni pamoja na wanafunzi kulipwa stahili zao na mamlaka husika. Jumuiya hiyo imegundua kwamba mamlaka zilizopewa dhima ya kuhudumia elimu ya juu na kutatua matatizo ya wanafunzi hao hazifanyi hivyo hadi pale wanafunzi hao wanapotishia kuandamana nchi nzima. Ni utamaduni mpya unaotumiwa na baadhi ya viongozi wetu, kwamba wanafunzi, wakulima, madaktari na wananchi wengine watalipwa madai yao iwapo tu watafanya vurugu au kuandamana na kuitikisa dola.

Hivyo ndivyo ilivyotokea katika suala la madai ya wanafunzi hao ya kulipwa fedha za mafunzo kwa vitendo. Hivi sasa wanafunzi kutoka katika vyuo vya elimu ya juu wako sehemu mbalimbali nchini katika mafunzo kwa vitendo, lakini wanafunzi kutoka vyuo saba hawajalipwa fedha za kujikimu. Wanaishi vipi katika mazingira mageni wakiwa hawana fedha za chakula au malazi ni swali ambalo halina jibu. Viongozi wa Tahliso wamesema ucheleweshwaji wa fedha hizo zinazokadiriwa kuwa Sh6.6 bilioni umesababisha baadhi ya wanafunzi wa kike kudhalilishwa kimapenzi na kutupiwa vyombo vyao nje kwenye nyumba walizopanga.

Kutokana na hali hiyo, viongozi wa Tahliso walipanga kuongoza maandamano keshokutwa kwenda kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda hata kama maandamano hayo yangekosa kibali cha polisi. Pamoja na viongozi hao kukamatwa na polisi na baadaye kuachiwa kwa dhamana, walisisitiza kwamba lazima maandamano hayo yafanyike kwani Tahliso inasimamia haki za wanafunzi ambazo Serikali imeshindwa kuzishughulikia. Msimamo huo uliizindua Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB), ambayo ilitangaza jana katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa, wanafunzi hao watakuwa wamelipwa fedha zao ifikapo wiki ijayo.


Maelezo ya bodi hiyo kuhusu kucheleweshwa kwa fedha hizo yanachekesha. Eti fedha hazikuwapo ila sasa hundi imepatikana kutoka serikalini, lakini itabidi ipitie katika mlolongo wa taratibu za kibenki na wiki ijayo wanafunzi watawekewa fedha hizo katika akaunti zao. Fedha hizo zimecheleweshwa kwa wiki saba sasa na ndiyo maana tunajiuliza wanafunzi hao wameishi vipi kwa muda wote huo? Bila shaka wameishi maisha ya mateso, karaha na udhalilishaji. Kama Tahliso isingekakamaa na kuazimia kuandaa maandamano, bila shaka wanafunzi hao wangeendelea kuteseka, huku viongozi hao wakila raha katika ofisi zao zenye viyoyozi.

Tuliwahi kusema kupitia safu hii kwamba bodi hiyo haiwezi kufanya kazi zake kwa ufanisi kutokana na kasoro za kisera na kimuundo ambazo zinailazimisha kufanya kazi kama idara ya Serikali. Tunajiuliza kwa nini bodi hiyo haikufanya mawasiliano mapema na Tahliso kuijulisha kwamba fedha hizo zisingepatikana kwa wakati, ili zitafutwe njia mbadala za kuwasaidia wanafunzi hao? Mbona malipo ya wanasiasa yanapatikana haraka na kwa wakati? Kwa nini Serikali hailipi madeni mpaka wanaoidai wapange kuandamana barabarani? 

Sisi tunadhani kwamba wizara husika nayo imekuwa sehemu ya tatizo, kwani imeshindwa kuisimamia bodi hiyo ili itekeleze sheria zilizopitishwa na Bunge kuhusu mikopo ya wanafunzi. Tunaishauri Serikali iwekeze kwenye elimu badala ya siasa na itambue kwamba mafunzo kwa vitendo ndiyo hasa elimu yenyewe. Tunawapongeza viongozi wa Tahliso kwa kusimamia suala hilo ipasavyo. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...