Monday, August 04, 2014

SUMAYE ATAJA SIFA 10 ZA RAIS AJAYE...!!!

Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ametaja sifa 10 za mtu anayefaa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 akiwataka wananchi kuzizingatia na kutokubali kudanganyika.
Alisema mbali na sifa hizo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) inatakiwa kusimamia uchaguzi huo kwa haki na kuhakikisha kuwa daftari la kudumu la wapiga kura linafanyiwa maboresho ili kila Mtanzania apige kura kwa mujibu wa Katiba.
Sumaye alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa albamu Rose Muhando iitwayo ‘Kamata Pindo la Yesu’ katika Ukumbi wa Diamond Jubilee.
Sifa 10
Alisema sifa ya kwanza ni kuwa na kiongozi anayetambua, kuulinda na kuthamini umoja... “Kiongozi tunayemtaka lazima atambue hilo na awe tayari kuchukua hatua za kutuimarisha kuwa na nguvu zaidi za kiuchumi na kuimarisha muungano wetu na baadaye muungano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na hatimaye Afrika.” Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Alisema sifa ya pili, kiongozi lazima awe wa watu wote na anayejiamini kwa maelezo kuwa mtu wa aina hiyo anakuwa na uelewa thabiti wa kujua matatizo na matarajio ya anaotaka kuwaongoza.
“Sifa ya tatu ni uadilifu, kiongozi mwadilifu ni yule ambaye hupenda kutenda haki na kuhakikisha anaowaongoza wanatenda na wanatendewa haki ipasavyo kutoka kwa wote wanaotakiwa kutoa hizo haki.
Alitaja sifa ya nne kuwa kiongozi anayepiga vita rushwa na maovu mengine kama ufisadi, matumizi ya dawa za kulevya, mauaji na ujambazi na asiwe mfanyabiashara.
“Hivi mtu akiingia Ikulu kwa kununua wapiga kura akifika huko kazi yake ya kwanza itakuwa nini? Kwa vyovyote atarudisha kwanza fedha alizowahonga na atafanya hivyo kwa kupokea rushwa kutoka kwa matajiri wanaotaka huduma au mali za nchi yetu,” alisema.
Alisema sifa ya tano ni awe kiongozi atakayepiga vita umaskini kwa kuweka mipango thabiti ya kusimamia rasilimali za nchi. “Kiongozi tunayemtaka lazima awe na uwezo wa kuwa na serikali inayoweza kujadiliana na wawekezaji ili rasilimali zetu ziwanufaishe na Watanzania.”
Alisema sifa ya sita ni kiongozi atakayeweza kuboresha huduma za jamii kutokana na nchi hivi sasa kuwa na utaratibu usioridhisha wa upatikanaji wa huduma za afya, hasa kwa wajawazito na watoto.
“Saba, tunahitaji kiongozi mwenye nidhamu na utendaji wake wa kazi. Kuna tatizo kubwa la kushuka kwa nidhamu katika kazi hasa sekta ya umma na kusababisha shughuli ndogo kufanywa kwa muda mrefu. Hali hii inafanya sekta nyingi kudorora,” alisema.
“Sifa ya nane ni kuwa na kiongozi atakayeweza kusimamia mapato na matumizi ya fedha za umma. Kodi itumike kuboresha huduma za jamii, kulipia gharama za uendeshaji serikali, kugharimia miradi ya maendeleo.”
Alisema sifa ya tisa, ni kiongozi atakayeweza kukuza uchumi imara kwa maelezo kuwa nchi bila kuwa na uchumi imara matatizo mengine kama umaskini, ukosefu wa ajira, huduma mbovu za jamii, utegemezi kwa mataifa mengine, yataendelea bila kikomo.
“Sifa ya 10 ni kiongozi mzalendo anayejali masilahi umma kwanza kabla ya kitu chochote. Kiongozi mzalendo ataijali nchi yake na kuwainua Watanzania wote kwa kadri inavyowezekana ili wawe na maisha bora,” alisema.
Kuhusu uchaguzi mkuu, Sumaye alisema Watanzania wanatakiwa kuiombea nchi yao amani na kuitaka Nec kuhakikisha kuwa inaboresha daftari la wapiga kura ili kuondoa mvutano katika uchaguzi na kutoa haki sawa kwa vyama vya siasa katika kampeni za uchaguzi. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...