Sunday, January 12, 2014

CHAMA KIPYA CHA SIASA CHAJA, WALIOFUKUZWA WATAJWA KUKIANZISHA


MSA 775c5
*Chadaiwa kuundwa na waliofukuzwa upinzani
WAKATI fukuto la kufukuzwa uanachama kwenye Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) likiwa bado bichi, chama kipya cha siasa kimeanzishwa na watu wanaodaiwa kuwa ni muungano wa wanachama waliofukuzwa kutoka vyama vya upinzani nchini.

Taarifa zilizotufikia na kuthibitishwa na Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini, zinakitaja chama hicho kuwa ni African Alliance for Change and Transparence (AACT) na kwamba mipango ya usajili wa muda wa chama hicho inadaiwa kuanza kuratibiwa kwa takribani mwezi mmoja sasa.
Chama hicho kimekamilisha baadhi ya taratibu na kinatarajiwa kupewa usajili wa muda na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa siku ya Jumanne, wiki ijayo.
Upo uwezekano wa wanachama waliofukuzwa uanachama kutoka Chadema hivi karibuni kujiunga na chama hicho. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz
Wanasiasa wengine wanaotajwa ama kuwa nyuma ya kuanzishwa kwa chama hicho au wanatarajia kujiunga, ni wale waliofukuzwa kutoka CUF, nia ikiwa ni kuendeleza harakati zao za kisiasa.
Mmoja wa watu wanaounda chama hicho alilidokeza gazeti hili kuwa endapo chama hicho kitapata usajili baada ya hapo, taratibu na harakati za kuanza kukitangaza zitafanyika katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema pia wamepanga kuendesha siasa zenye upinzani, ikiwa ni pamoja na kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2015 iwapo kitakuwa tayari kimejiimarisha.
Hivi karibuni Kamati Kuu Chadema, iliwavua uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo, huku Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, akikimbilia Mahakamani kuomba zuio la kutojadiliwa uanachama wake na kikao hicho.
Zitto, Dk. Kitila na Mwigamba walituhumiwa na uongozi wa juu wa Chadema kuandaa waraka wa siri wenye lengo la kufanya mabadiliko ya uongozi ndani ya chama, hali iliyoibua mgogoro mzito hadi kufikia uamuzi wa kuwavua uanachama baadhi yao.
Alipoulizwa Dk. Kitila kama ameshiriki na wenzake kuanzisha chama cha siasa, alishindwa kukataa wala kukubali, kwa kusema kuwa ukweli ama uongo wa habari hiyo utajulikana.
Alipotajiwa chama hicho na kwamba kinatarajia kupata usajili wa muda, alisema hafahamu hilo na hawezi kuzungumzia.
"Sina cha kuzungumza juu ya swali lako, kuwapo kwa chama kipya au la, nadhani ukweli utajiweka wazi nanyi mtabaini tu, hata hilo jina la chama kipya kuitwa AACT sijui," alisema Dk. Kitila.
Mpaka sasa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu nchini ni 23, ambavyo ni CCM, CUF, Chadema, UMD, NCCR-Mageuzi, NLD, UPDP, NRA, Tadea.
Vingine ni TLP, UDP, Demokrasia Makini, Chausta, DP, APPT-Maendeleo, Jahazi Asilia, Sau na AFP, UMD, FORD, CCK, ADC na Chaumma. Chama: 
Na Mtanzania

Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...