Thursday, November 07, 2013

WAPINGA MAREKEBISHO SHERIA YA MAGAZETI


lissu_5a412.jpg
Wakati Serikali imewasilisha muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Magazeti, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imepinga marekebisho ya sheria hiyo kwa madai kuwa hayakufanyiwa tafakuri na utafiti.
Akiwasilisha maoni hayo bungeni jana, Msemaji wa Kambi hiyo kuhusu Sheria, Tundu Lissu, alisema mapendekezo hayo yamefikishwa bungeni bila kufanyia tafakuri au utafiti wowote.
"Mwanasheria Mkuu wa Serikali angefanya utafiti kidogo tu angegundua kwamba kifungu cha 55 hakina na hakijawahi kuwa na, sababu yoyote ya kuendelea kuwepo katika kanuni ya adhabu,"alisema .
Alisema hiyo inatokana na kifungu hicho hicho kutungwa upya, kwa maneno yale yale, kama kifungu cha 31 cha Sheria ya Magazeti kwamba kifungu hicho hakikupaswa kuwepo kwa sababu, makosa ambayo kifungu hicho kinafafanua hayako tena kwenye kanuni ya adhabu na badala yake, yako katika Sheria ya Magazeti.
"Inaelekea katika fasta fasta ya kupitisha muswada wa Sheria ya Magazeti, kifungu cha 55 kilisahauliwa katika kanuni ya adhabu wakati vifungu vyote vinavyohusu makosa ya uchochezi na kashfa ya kijinai vilipohamishiwa katika Sheria ya Magazeti,"alisema Lissu.
Alisema kwa sababu hiyo kambi yake inapendekeza kwamba mapendekezo ya aya ya 47 ya muswada huo yaondolewe.
"Na sasa, kwa muswada huu, badala ya kupendekeza sheria hii ifutwe kama ilivyokuwa kwa Sheria ya Shihata na kama ilivyopendekezwa na Tume ya Nyalali, Serikali hii ya CCM inaliomba Bunge lako tukufu kuiongezea makali zaidi," alisema.
Awali akiwasilisha muswada huo bungeni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, alisema muswada huo unapendekeza kuongeza adhabu ya faini kwa makosa ya kuchapisha habari za uchochezi ama habari inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Jaji Werema alisema hivi sasa adhabu ya makosa hayo ni Sh 150,000 ambayo ni ndogo ikilinganishwa na madhara ya kosa husika kwa jamii.
"Muswada unapendekeza katika ibara ya 40 na 41 kuwa vifungu hivyo virekebishwe kwa lengo la kuongeza adhabu ya faini kwa makosa hayo ili adhabu hiyo isizidi Sh5 milioni," alisema.
Jajin Werema alisema marekebisho hayo yanalenga katika kutekeleza azimio la Bunge katika mkutano wa 11 kikao cha 21, ambapo pamoja na mambo mengine Serikali ilitakiwa kupitia sheria zilizopo ili kuona kama zinatosheleza kuzuia lugha au kauli za uchochezi.
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, iliunga mkono marekebisho hayo yanayolenga kuongeza adhabu kwa makosa ya kutumia lugha za matusi na uchochezi unaoweza kusababisha machafuko.
Wanasheria walonga
Baadhi ya wanasheria waliozungumza na gazeti hili wamesema marekebisho yanayofanywa na Bunge, hayana maana kwa sasa na badala yake, sheria nzima inapaswa ifutwe kwa sababu
hailengi kujenga bali kuvibana vyombo vya habari.
Mwanasheria wa kujitegemea, Aloyce Komba alisema ni wakati mwafaka wa Serikali kurejea na kuridhia mapendekezo ya Tume ya Jaji Nyalali ya kuzifuta sheria 40 zilizoainishwa na tume yake.
Alisema miongoni mwa sheria 40 zilizopendekezwa kufutwa na Jaji Nyalali, ni sheria ya magazeti ya mwaka 1976.
Ofisa Habari wa Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Afrika, Wakili Hamza Abbas, alisema endapo Serikali inafanya marekebisho ya vifungu ambavyo havitajwi katika kesi au shauri lililopo mahakamani, inakuwa haijaingilia mahakama.
Chanzo:Mwananchi

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...