Thursday, November 07, 2013

MBUNGE WA UKEREWE AFUTIWA DHAMANA NA KUAMRIWA AENDE SELO SIKU 14

560843761_fd884.jpg
Na mwanahabari Bundala William
DHAMANA ya mbunge wa jimbo la Ukerewe, Salvatory Machemli (CHADEMA) imefutwa na ameamuriwa na mahakama kwenda rumande siku 14 kwa kuwa wadhamini wake wamekosa sifa baada ya mshitakiwa na wadhamini wake watatu kushindwa kufika mahakamani ili kuwezesha kesi inayomkabili kusikilizwa kama ilivyopangwa.
Pia, Mbunge huyo ametakiwa kuwasilisha vitambulisho vyake katika kituo cha polisi na amezuiliwa kutoka nje ya wilaya bila kibali cha mahakama.
Hakimu mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya hiyo Faustine Kishenyi ametoa uamuzi huo leo baada ya upande wa mashitaka kuomba mshitakiwa afutiwe dhamana.


Wadhamini ambao ni Shellifu Ngelezya, Max Mhogo na Konsolata Machemli wamepoteza sifa hivyo udhamini wao umefutwa.
Mwendesha mashitaka wa jeshi la polisi, Inspekta Samweli Onyango amesema mshitakiwa kwa makusudi ameshindwa kufika mahakani zaidi ya mara tano bila kutoa taarifa wakati kesi yake ikitajwa.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, hakimu huyo aliamuru mmoja wa wadhamini wake, Max Mhogo, awekwe rumande siku saba na baada ya kutoka alitakiwa leo (Novemba 6) afike mahakamani hapo na mshitakiwa pamoja na wadhamini wake.
Katika utetezi wake, Machemli amesema ameshindwa kufika mahakani kama ilivyopangwa kwa sababu ya tarehe ya kesi yake kuingiliana na vikao vya Bunge.
Kesi hiyo imeahirshwa hadi tarehe 20 mwezi huu .
Mbunge huyo anakabiliwa na kesi ya uchochezi.
Mwendesha mashitaka wa polisi, ASP Denis Rwiza alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa linalomkabili, Oktoba 23, 2011 katika Kijiji cha Nyamanga kisiwani Ukara wakati akiutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CHADEMA.
Alisema mshitakiwa huyo kwa makusudi aliwachochea wananchi kutenda kosa la shambulio kwa kuwaelekeza wachukue uamuzi mgumu wa kuwazuia, hata kushambulia kwa silaha za jadi ikiwemo marungu, mapanga na fimbo afisa yeyote wa polisi atakayekwenda kutafuta watuhumiwa nyakati za usiku kisiwani hapo.
Katika maelezo yake, mwendesha mashitaka huyo wa polisi alisema kipindi hicho ulikuwepo msako wa watuhumiwa wa mauaji ya watu wanne waliouawa na wananchi Desemba 10, 2010 mbele ya maofisa wa polisi kwa tuhuma za ujambazi.
---
Taarifa wavuti.com ilizozipata jioni hii zinasema kuwa tayari Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mhe. Freeman Mbowe amemwandikia rasmi baruaKatibu wa Bunge kumjulisha juu ya jambo hili na wananchi wanaendelea kutafuta dhamana ili kukidhi masharti yaliyowekwa ikiwa ni pamoja na wadhamini watatu na hati tatu za nyumba.
Source: wavuti.com

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...