Tuesday, September 10, 2013

SERIKALI YAKUSUDIA KUANZISHA MTIHANI WA TAIFA WA DARASA LA PILI...!!!



Mtihani mpya wa Taifa utaanzishwa kwa wanafunzi wa darasa la pili nchi nzima, ili kuchuja watakaoshindwa kusoma, kuandika na kuhesabu.

Akifafanua uamuzi wa kuanzishwa mtihani wa Taifa wa darasa la pili, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema mtihani huo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa matokeo makubwa sasa katika sekta ya elimu.

Malengo ya mtihani huo kwa mujibu wa Mulugo ni kuondoa uwezekano wa kuwa na wanafunzi katika madarasa ya juu, wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu na ili kufikia malengo hayo, watakaoshindwa 
mtihani huo, watarudia mpaka wajue kusoma na kuandika.


Aprili mwaka jana, Mulugo alipokuwa akizungumza na   wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), alikaririwa akikiri kuwa katika mtihani wa Taifa wa kumaliza elimu ya msingi  wa mwaka juzi, kulikuwa na wanafunzi wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu, waliochaguliwa kujiunga na sekondari.

Kutokana na udanganyifu katika mitihani ya Taifa, Mulugo alikaririwa akiagiza wanafunzi walioingia kidato cha kwanza wapimwe uwezo wao wa kusoma na kuandika na kuhesabu.

Alikaririwa akisema kwa mujibu wa tathmini, mkoa wa Kilimanjaro uliongoza kwa kuwa na wanafunzi wengi wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu.

"Mkoa wa Kilimanjaro una wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika wapatao 660, Tanga 490 na Dar es Salaam 208," alikaririwa Mulugo bila kutaja matokeo ya mikoa mengine.

“Hili ndilo janga la kitaifa sasa. Si hayo mengine ambayo watu wanasema ni majanga ya kitaifa. Lazima tujiulize kwa nini watoto wanamaliza darasa la saba wakiwa hawajui kusoma na kuandika na wanafaulu?” Alihoji na kuongeza: “Je, siku hizi hakuna tena somo la kusoma na kuandika? Kwa nini mtoto amalize shule bila kuwa na maarifa ya KKK (Kusoma, Kuandika na Kuhesabu)?   Jambo la kusikitisha kuna mpaka baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tatu, ambao hawajui kusoma wala kuandika. Tulipofikia si pazuri hata kidogo, lazima tuwe makini jamani.  Tuheshimu Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), tupate ufumbuzi wa mambo haya, Taifa hili ni letu sote, lazima tuhakikishe linasimama imara,” alikaririwa Mulugo.
 via HabariLeo

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...