Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limelazimika kufunga transfoma zisizotumia mafuta kutokana na tatizo kubwa la wizi wa mafuta ya transfoma kwa maeneo mengi nchini.
Meneja mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud amesema, shirika hilo limelazimika kufunga transfoma zijulikanazo kama ‘Dry type Transfoma’ambazo hazitumii mafuta ili kupambana na changamoto za wizi wa mafuta unasababisha baadhi ya maeneo kukosa umeme.
“Tatizo la wizi wa mafuta ya Transfoma ni kubwa, limesababisha shirika kununua transfoma zisizotumia mafuta ambazo zinapatikana kwa gharama kubwa ukilinganisha na transfoma zitumiazo mafuta ili kuepusha kutokukatika kwa umeme kwa maeneo husika,” alisema Badra
Aliyataja baadhi ya maeneo ambayo yamefungwa transfoma zisizotumia mafuta kutokana na kukithiri kwa tatizo la wizi huo kuwa ni pamoja na Mbezi Beach na maeneo mengi katika Wilaya ya Temeke.
Aliongeza, Tanesco kupitia walinzi wake wanaozungukia maeneo ya transfoma, wamekamata baadhi ya watu na kuwafikisha katika mikono ya sheria ambapo wengi wao wamefungwa, pia wameomba msaada toka ulinzi shirikishi ili kuzidi kuwakamata vishoka hao ambao wanasababisha wananchi kukosa umeme na shirika kukosa mapato.
Pia alionya wezi wa nyaya za umeme hususan za copper, pamoja na wapandaji miti chini ya nguzo kama moja ya watu wanaodidimiza shirika kwa kusababisha hasara za kila siku zinazoweza kuepukika.
Badra alisema, “ili shirika liendelee ni lazima jamii itupe ushirikiano kwa kulinda miundombinu ya Tanesco, pia iwataje wahusika wanaoharibu pamoja na kuiba’’.
HABARI LEO