Rais aliyasema hayo katika uwanja wa Kaitaba alipokuwa akihitimisha ziara yake mkoani Kagera aliyoanza Jumatano wiki iliyopita.
“Mbunge na Meya wakiendelea kutiliana shaka wanaoumizwa ni wananchi, malizeni tofauti zenu kwa sababu hakuna lisilokuwa na mwisho,” alisema.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema masuala yaliyokuwa yakiwagonganisha Meya na Balozi Kaghasheki ambaye ni Mbunge wa Bukoba Mjini, ya ujenzi wa soko pamoja na viwanja ni mambo ya maendeleo.
Katika ugomvi huo, Kaghasheki anapinga ujenzi wa soko jipya mjini Bukoba kwa madai kwamba haukufuata maamuzi ya vikao vya Baraza la Madiwani wakati Meya akisisitiza ujenzi huo kwa maelezo kwamba maamuzi ya ujenzi yamepitishwa kwenye vikao vya baraza la madiwani.
Rais Kikwete alisema ujenzi wa soko ni suala la maendeleo lakini akataka Manispaa iwatafutie eneo wajasiriamali wanaoendesha biashara zao kwenye soko la sasa ambalo litavunjwa na kujengwa jipya.
Rais Kikwete aliagiza kuwa baada ya ujenzi, wananchi wanaondesha biashara zao katika soko hilo wapewe kipaumbele.
“Ujenzi wa soko ni maendeleo na karne hii ni ya teknolojia, ni uamuzi mwema; mkitaka mambo ya zamani basi na nyinyi mtakuwa ni watu wa kizamani,” alisema.
“Katika mradi huu mpya wa viwanja 5,000 kwanza wapeni hao 800 wa zamani maana walikwishalipia hilo ni deni la manispaa wala haliwezi kukwepeka hata kama viongozi wa sasa hawakuwapo wakati huo,” alisema Rais Kikwete.
No comments:
Post a Comment