Rais
Kikwete akitoa heshima za mwisho kwa marehemu askari waliouwawa huko
Darfur wakitekeleza majukumu ya umoja wa mataifa ya kulinda amani.
Dar es Salaam.
Rais
Jakaya Kikwete ameutaka Umoja wa Mataifa (UN), kuruhusu kutumika kwa
mtutu katika operesheni za kulinda amani zinazoendelea.
Alitoa
kauli hiyo jana baada ya kutoa heshima zake kwa wapiganaji saba wa
Tanzania waliokuwa Darfur, Sudan katika operesheni ya kulinda amani ya
UN na Afrika (Unamid) ambao waliuawa na kundi linalodaiwa la wanamgambo
wa Janjaweed wanaoungwa mkono na Serikali ya Sudan inayoongozwa na Rais
Omar al-Bashir.
Wapiganaji waliouawa ni Oswald Chaula kutoka 42KJ
Chabruma, Songea, Peter Werema (44KJ Mbeya), Fortunatus Msofe (36KJ
Msangani, Pwani), Rodney Ndunguru (92KJ Ngerengere), Mohamed Juma (94KJ
Mwenge), Mohamed Chukilizo (41KJ Nachingwea) na Shaibu Othman (MMJ-
Upanga).
“Lazima nikiri kuwa taarifa hiyo ya vifo vya vijana wetu
ilinihuzunisha, kunisikitisha na kunikasirisha. Kwa nini watu wa Darfur
wawaue wanajeshi wetu ambao wamekwenda kule kuwasaidia wapate utulivu
ili kunusuru maisha yao, kuwaondolea wasiwasi na kuwawezesha wafanye
shughuli zenye tija kuendesha maisha yao?
“Moja kwa moja sikusita
kuamini kuwa waliofanya hivyo ni watu wahalifu. Tangu uhuru ni sera ya
nchi yetu kutetea wanyonge dhidi ya ukoloni, ubaguzi, uonevu, dhuluma na
watu wote walioko katika mazingira hatarishi Afrika na duniani. UN
ifanyie marekebisho sheria ili majeshi yanayolinda amani yawe na nguvu
za kujihami ili kuzuia maafa yanayoweza kujitokeza.”
Hivi
karibuni, Msemaji wa Unamid, Chris Cycmanik alimwambia mwandishi wetu:
“Majeshi ya UN mjini Darfur yanaweza kufanya kazi chini ya Kifungu cha
VII ambao inaruhusu kutumia nguvu lakini kwa hali iliyopo hawafanyi
hivyo,” alisema.
Rais Kikwete alisema eneo hilo ni hatarishi kwa
sababu hadi sasa watu 41 kutoka katika nchi mbalimbali wameuawa wakati
wakilinda amani huku wengine 55 wakijeruhiwa tangu mpango wa kulinda
amani ulipoanza mwaka 2007.
“Tumeshawasilisha UN maombi kutaka
Kifungu namba Sita cha kulinda amani kibadilishwe na kitumike Kifungu
namba Saba ambacho kinawataka askari kujihami pindi wanapovamiwa na
maadui,” alisema.
Alisema tayari amewasiliana na Rais al-Bashir
akimtaka kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua kali wote waliohusika
na tukio hilo huku akiwataka wanajeshi kutokata tamaa kwa tukio hilo na
kulichukua kama changamoto katika kujilinda na kuwabaini maadui.
Aliwapa
pole wafiwa na kusema Serikali na wananchi wote wapo pamoja katika
kipindi hiki kigumu na kuwataka kuwa na subira. Waziri wa Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha alisema kitendo cha waasi
kuwaua wanajeshi saba wa Tanzania ni mkakati wa vikundi vya waasi
kuhakikisha kuwa jitihada za kuleta amani zinagonga mwamba.
Mkuu
wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jenerali Davis Mwamunyange
alisema askari hao pamoja na wengine walikuwa wakisindikiza msafara wa
walinzi wa amani uliokuwa ukitoka katika kambi yao karibu na Mji wa
Nyala.
Alisema walipofika kilometa 25, katika eneo la Khor Abeche
walivamiwa kwa kushtukizwa na kikundi cha watu wachache na kwa sababu
hawakuwa na silaha za kujihami, walishindwa kujitetea na kusababisha
vifo hivyo.
Simanzi, vilio vyatawala
Rais
Kikwete aliwasili katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa saa
11.10 asubuhi na kupokewa na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal,
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na
Jenerali Mwamunyange.
Muda mfupi baadaye, malori saba kila moja likiwa na mwili wa wanajeshi hao yaliwasili katika viwanja vya wizara hiyo.
Wakati miili hiyo ikiteremshwa kwa ajili ya kuaga, wafiwa ambao awali, walikuwa wametulia kwenye viti walianza kulia.
Rais na mkewe, Salma walianza kutoa heshima zao na kisha kuwapa mkono wa pole wafiwa.
Askari
wawili wa JWTZ walizirai wakati utoaji huo wa heshima za mwisho
ukiendelea na walibebwa na wenzao kwenda kupatiwa huduma ya kwanza.
Mamia
ya wakazi wa Dar es Salaam walijitokeza katika viwanja hivyo kiasi cha
wengine kukosa nafasi ya kuingia ndani hivyo kulazimika kukaa nje hadi
miili hiyo ilipoondoshwa tayari kwa kusafirishwa sehemu mbalimbali kwa
maziko.
Ndugu
na jamaa wa askari saba wa Tanzania waliokuwa katika Jeshi la Kulinda
Amani la Umoja wa Mataifa na Afrika (Unamid), waliouawa huko Darfur,
Sudan wakiwa na simanzi wakati wa kutoa heshima za mwisho katika Viwanja
vya Makao Makuu ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dar es
Salaam jana.
No comments:
Post a Comment