CHAMA cha demokrasia na Maendeleo (Chadema),
kimetangaza kuanza kutoa mafunzo ya kujihami kwa vijana wao maarufu kama Red
brigedi kuanzia Agosti mosi, mwaka
huu.
Akitangaza tarehe hiyo jana wakati wa mkutano wa chama
hicho uliofanyika Mbalizi wilaya ya Mbeya Vijijini, kiongozi wa ulinzi wa chama
hicho kanda ya Nyanda za juu kusini Lucas Mwampiki, alisema kuwa ameamua kuweka
wazi adhima hiyo ili serikali isiendelee kusumbuka kuwa inao uwezo wa
kuwazuia.
‘’Polisi msisumbuke
kutafuta kuwa tutaanza lini, ni hivi, tutaanza tarehe 1, mwezi wa nane mwaka
huu’’ alisema Mwampiki ambaye pia ni diwani wa kata ya Mwakibete
Jijini Mbeya.
Mgeni rasmi katika mkutano
huo Godbless Lema ambaye ni Mjumbe wa kamati kuu ya Chadema na Mbunge wa Arusha
mjini, alisema amekuwa akipokea simu nyingi kutoka kwa vijana waliohitimu
mafunzo ya JKT na kuachwa bila ajira ili wajiunge na mafunzo
hayo.
‘’Nimekuwa nikipokea simu nyingi za vijana waliohitimu JKT
na kuachwa mitaani wakiomba kujiunga na mafunzo ya Redbrigedi huku wakiuliza
kiingilio’’ alisema Lema.
Alisema kuwa ijulikane kuwa
mtu anapozuia demokrasia anazalisha waasi na Chadema hawapo tayari kuuawa
kijinga.
Mbali na suala hilo, Lema
alisema alishangazwa na uandishi wa vyombo vya habari hapa nchini katika ujio wa
Rais wa Marekani Barack Obama, ambapo Magazeti
mengi yaliandika habari za kushikana viuno na mkewe badala ya kuandika jambo
ambalo aliloijia.
‘’Waandishi wa Tanzania badala ya kuandika alichojia
Obama, wao waliishia kupiga picha akiwa ameshikana na mkewe na kuweka front page
huku madini yakiondoka na Rais Kikwete akiongoza
kuomba Kondomu na kusaini mikataba ya kutorosha madini
yetu’’alisema Lema huku akishangiliwa na wananchi zaidi ya 2000
waliohudhuria mkutano huo wakiwemo viongozi wa CCM.
Aliwaambia wanachama wa
Chadema kuwa waache kuwachukia wanachama wa CCM bali wawaelimishe taratibu maana
hata ukitaka kupata kifaranga huwezi kununua yai dukani na kulipasua kisha
ukapata kifaranga bali mpaka yai hilo liatamiwe na
kuangaliwe.
Mbunge wa Mbeya Mjini
Joseph Mbilinyi, alisema kwa sasa anakubali kuwa yeye ni ‘’Rais wa Mbeya’’
kutokana na wananchi kumkubali na kwamba CCM wasitarajie kulikomboa Jimbo la
Mbeya Mjini mwaka 2015 na aliwashukuru sana Polisi wa Mbeya kwa kuacha kuisaidia
CCM.
Mwenyekiti wa kamati ya
maandalizi ya mkutano huo wa kuimarisha chama katika kata ya Nsalala na Utengule
Usongwe Kissman Mwangomale (KK) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha
Mshikamano kata ya Nsalala, alisema kuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda anapaswa
kujiuzulu kwasababu alitamka kuwa amechoka.
‘’Pinda anapaswa
ajiuzulu maana alitamka kuwa amechoka, sisi hatujachoka tuna uwezo wa kuongoza
dola aachie ngazi au afute haraka kauli yake’’ alisema
Mwangomale.
Naye diwani wa kata ya
Iyela ya Jijini Mbeya Charles Mkela, aliwashukuru wanachama wa CCM kumpigia kura
nyingi za ndiyo katika uchaguzi mdogo uliofanyika hivi karibuni na kukiwezesha
Chadema kushinda.
Mkutano huo ulihudhuriwa na
viongozi mbalimbali wa Chadema akiwemo Frank Mwaisumbe ambaye ni Mratibu wa
Chadema kanda ya nyanda za juu kusini na viongozi kutoka Mbeya mjini na wilaya
ya Mbozi.
No comments:
Post a Comment