Obama: Tunataka Uwazi wa Mikataba. Omba radhi Kwa mauaji ya Lumumba
Hatimaye Barack Obama, Rais wa Marekani anatembelea tena bara la
Afrika. Hii itakuwa ni mara ya pili Obama kutembelea Bara hili alikotoka
baba yake baada ya ziara yake ya kwanza mwaka 2009. Mwaka huo
alitembelea Ghana na Misri ilhali mwaka huu anatembelea Senegali, Afrika
Kusini na Tanzania. Ziara hiyo itakayoanza tarehe 26 mwezi Juni,
itamfikisha Tanzania tarehe 1 Julai na kuondoka siku ya pili yake.
Uchaguzi wa Obama kuwa Rais wa Marekani ulipokolewa kwa shangwe Afrika
nzima. Wakati Waziri wa mambo ya nje wa Nigeria alilia kwa furaha,
nchi ya Kenya ilitangaza siku ya mapumziko na Rais wa zamani wa Afrika
Kusini ndugu Nelson ‘Madiba’ Mandela alisema ‘ushindi wa Obama
unawafanya Waafrika wathubutu kuota ndoto (Jarida la The Economist).
Hapa Tanzania kulikuwa kuna shamra shamra za kila namna na magazeti
yaliweka vichwa vya habari kana kwamba ni Rais wa Tanzania
aliyechaguliwa.
Waafrika walikuwa na matumaini makubwa sana na bwana Obama. Yamefikiwa?
Ni vema ifahamike kuwa Barack Obama ni Rais wa Marekani na siku zote
atalinda maslahi ya Marekani tu. Kuwa na matumaini makubwa kwamba labda
yeye angeliweza kuiweka Afrika mbele sana ilikuwa ni kujifurahisha tu
nafsi. Maslahi ya Marekani ni ya kipaumbele kuliko kitu kingine chochote
kwa Rais Obama. Kwa wengi Obama amekuwa kama amewavunja moyo.
Tanzania inapokea kiongozi wa Taifa kubwa duniani wa pili sasa ndani
ya kipindi cha miezi 3 tu. Kwanza alikuja Rais wa China na sasa wiki
hii anakuja Rais wa Marekani. Maneno ya mtaani na kwenye mabaraza ya
majadiliano ni kwamba viongozi hawa wanakuja kugombea maliasili tulizo
nazo kama gesi asilia na madini. Nadhani haya ni maneno ya kusema katika
kupiga soga maana kunyonywa kwa rasilimali hakuhitaji Rais wa Marekani
aje Tanzania. Makampuni yote makubwa yanayochimba dhahabu hapa nchini
ni makampuni ya nje na marais wao hawakuja ili waweze kupata mikataba
minono ya kuvuna utajiri wetu. Katika kitalu namba 2 cha utafutaji wa
mafuta na gesi huko Bahari Kuu kampuni ya kimarekani ya ExxonMobil ina
ubia na kampuni ya Norway ya StatOil. Kampuni hiyo haikusubiri Rais wa
Marekani aje ili wapate mikataba.
Kuna makampuni mengi sana
ya kichina yanajenga barabara zetu hapa nchini yakiwa na mikataba
minono sana. Kule Mchuchuma na Liganga kuna kampuni ya kichina
inajiandaa na uchimbaji wa chuma na makaa ya mawe. Makampuni yote haya
hayakusubiri Rais wao aje.
Hoja inayojengwa hapa ni kwamba
ujio wa Marais mbalimbali nchini ni ujio wa kujijenga kidiplomasia na
wakati mwingine kama sehemu ya kutuma ujumbe Fulani kwa dunia. Nchi
inayotembelewa pia inaweza kuona kuwa diplomasia yake inaheshimiwa na
mataifa yanayoitembelea.
Hata hivyo hii haiondoi ukweli
kwamba Obama anakuja kwa ajili ya maslahi ya nchi yake kama ilivyo kwa
wachina walivyokuja. Tumesikia Rais Obama ataambatana na mamia ya
wafanyabishara kutoka Marekani kwa ajili ya kupata fursa za kuwekeza
nchini. Pia tutasikia matangazo kuhusu msaada wa pili wa Millenium
Challenge ambapo Wamarekani wanaendelea kumwaga pesa nchini kusaidia
miundombinu lakini pia kushawishi kuungwa mkono na nchi zetu kwenye
maamuzi Fulani Fulani jumuiya za kimataifa.
Tumesikia Obama
atakwenda kutembelea mitambo ya kampuni ya Symbion. Hii ni mitambo
ambayo miaka 4 iliyopita ilipigiwa kelele kuwa ni mitumba na hivyo
TANESCO wasiinunue. Hawakununua na badala yake kampuni hiyo ya
kimarekani ikainunua, wakaingia mkataba na TANESCO kuwauzia umeme
unaozalishwa na mitambo hiyo hiyo chakavu. Wakati tunasuburi kulipa
takribani tshs 105 bilioni kwa Dowans baada ya kutubwaga kwenye kesi,
tunasubiri kuona wanasiasa watakaokwenda kumsindikiza Obama kwenye
matembezi hayo ya kutembelea mitambo chakavu.
Kampuni kubwa
ya kutengeneza mitambo ya kuzalisha umeme ya GE imetangaza kuingia ubia
na kampuni ya Symbion kuzalisha umeme nchini. Takribani 400MW
zitazalishwa kutoka Mtwara na kuingizwa kwenye gridi ya Taifa. Pia
sehemu kubwa ya umeme utakaozalishwa Mtwara tayari umepata soko kwenye
kiwanda cha kuzalisha udongo ulaya (simenti) cha bwana Dangote kule
Mtwara. Mtendaji Mkuu wa GE bwana Jeff Immelt ametangaza kuwa kampuni
yake itauza mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi mingi zaidi
Afrika Mashariki kuliko Marekani katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Ni biashara tu!
Nishati naona ni kipaumbele kikubwa sana kwa
ziara ya Rais Obama. Kwa nchi kama yetu yenye watu asilimia 21 tu
wenye umeme, ni dhahiri kipaumbele hiki watu wengi watakiiunga mkono.
Hata hivyo Obama ni lazima asimame kidete kuhakikisha kuwa kampuni za
nchini mwake zinazopata miakataba hapa nchini ziweke wazi mikataba hiyo
na kulipa kodi inavyostahili. Makampuni ya mafuta kutoka Marekani
hayana historia nzuri duniani na hivyo ni lazima tulisisitize mapema
kabisa. Uwazi wa mikataba na uwezo wa kupambana na ukwepaji kodi ni
muhimu sana katika vita dhidi ya Ufisadi na ubadhirifu.
Rais
Obama atambue kuwa iwapo Tanzania ingekuwa inakusanya nusu ya kodi
zinazokwepwa na makampuni makubwa yanayotumia mbinu kali, basi
tungehitaji misaada ya Marekani na hapa nchini angekuja kama mbia wa
kweli na sawa katika dunia. Hivyo ni vema aungane na Waziri Mkuu wa
Uingereza kuhakikisha kuwa makampuni makubwa hayatumii ‘tax havens’
kukwepa kodi katika nchi kama Tanzania. Uwazi wa mapato yao na
kilicholipwa kwa Serikali ni vema usisitizwe sana na Obama mwenyewe ili
makampuni yao yasikie na yaache kupora utajiri wa Afrika kiujanja
ujanja.
Mwisho ni vema kama Rais Obama ataomba radhi kwa
ushiriki wa Marekani kwenye mauaji wa Waziri Mkuu wa kwanza wa Kongo
Patrice Lumumba. Hivi Tanzania inahangaika zaidi ya uwezo wake kupeleka
majeshi huko mashariki ya Kongo kulinda amani. Waafrika wengi
tunaamini kuwa mauaji ya Lumumba ilikuwa ni kama laana kwa Taifa lile
na hivyo limekuwa ni taifa la vurugu na vita licha ya utajiri mkubwa
ulioko nchini humo. Nyaraka za CIA zinaonyesha dhahiri kuwa Rais wa
Marekani wa wakati huo Lyndon Johnson aliagiza kuuwawa kwa
mwanamapinduzi Patrice Lumumba. Kuwaomba radhi Waafrika na hasa Wakongo
kuhusu mauaji ya Lumumba ni jambo litakaloweza kusaidia sana kurejesha
amani Kongo.
Karibu Afrika, Karibu Tanzania ndugu Barack Hussein Obama.
Zitto Z Kabwe
No comments:
Post a Comment