Tuesday, June 04, 2013

VITI MAALUMU VYAFUTWA, UBUNGE KUWA NA UKOMO


Tume ya Mabadiliko ya Katiba imependekeza katika rasimu ya Katiba Mpya ukomo wa wabunge na kufutwa kwa nafasi za Viti Maalumu bungeni.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mstaafu Joseph Warioba alisema jana, wanapendekeza kwamba ubunge uwe na ukomo wa vipindi vitatu vya miaka mitano, mitano akimaanisha kwamba kipindi cha mtu kuwa mbunge hakiwezi kuvuka miaka 15.

Rasimu hiyo ya Katiba imependekeza kutokuwapo tena kwa Viti Maalumu na badala yake, imetaka kuwapo kwa nafasi tano za uteuzi zibaki kwa Rais ambazo zitahusisha makundi maalumu ya watu wenye ulemavu pekee.

Jaji Warioba alisema Tume imependekeza kuwapo kwa
majimbo 25 ya uchaguzi kwa Tanzania Bara na 20 kwa Zanzibar ambayo kila moja litakuwa na wabunge wawili, mwanamke na mwanamume. Kwa mujibu wa rasimu hiyo, majimbo hayo ni mikoa 25 ya Tanzania Bara na wilaya 10 za Zanzibar. Kwa maana hiyo, Bunge la Muungano litakuwa dogo lenye wabunge 75.


Mwenyekiti huyo alisema, wananchi watakuwa na mamlaka ya kumwondoa madarakani mbunge wao endapo hawataridhishwa na utendaji kazi wake.

Alisema hakutakuwa na uchaguzi mdogo wa wabunge kwa wabunge watakaopitia kwenye vyama vya siasa na badala yake jimbo litakapokuwa wazi chama kilichokuwa kikiongoza kitateua atakayeshika wadhifa huo.

“Uchaguzi mdogo utafanyika pindi tu aliyekuwa akiongoza alitokana na mgombea huru (binafsi) hivyo, Tume huru ya Uchaguzi itatakiwa kuandaa uchaguzi mdogo,” alisema Jaji Warioba.

Kuhusu kiti cha Spika na Naibu Spika, alisema baada ya kupokea maoni na wananchi mbalimbali, Tume hiyo imependekeza viongozi hao wasitokane na vyama vya siasa.Alisema Tume inapendekeza Spika na Naibu Spika wasitokane na wabunge na wasiwe viongozi wa vyama vya siasa wala wasitokane na asasi za kiraia ambao wataidhinishwa na Bunge.

Wafurahia mapendekezo

Mkazi wa Uhindini, Mbeya, Boniface Mwakinga alisema amefurahishwa na mapendekezo yanayotaka kuwapo kwa ukomo wa madaraka ya wabunge.

Mfanyakazi wa Hospitali ya Kilema, Kilimanjaro, Dennis Mfumbulwa alisema kati ya mambo yaliyomgusa katika rasimu hiyo ni hatua ya wananchi kupewa nguvu ya kumwondoa mbunge ambaye hawajibiki kwa wapigakura wake akisema hilo sasa ni kitanzi kwa wabunge wababaishaji.

Mbunge wa Bunge la Afrika ya Mashariki, Shyrose Bhanji alieleza kufurahishwa kwake na kuondolewa kwa Viti Maalumu na kupendekezwa kwa utaratibu mpya wa kusimama na kugombea wanawake majimboni.
 “Lengo la kuanzishwa Viti Maalum ilikuwa ni kuwapa upendeleo maalumu wanawake kuingia katika siasa na vyombo vya uamuzi, nadhani imefanikiwa na sasa tunapaswa kushindanishwa sisi kwa sisi,” alisema Bhanji.


MWANANCHI

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...