Saturday, June 15, 2013

LOWASSA ATANGAZA NDOTO YAKE, ISOME HAPA

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akiwapungia mkono walimu walioshiriki katika hafla ya harambee ya kuchangia Saccos ya walimu iliyofanyika kwenye Viwanja vya Chuo cha Ushirika Moshi, jana. Picha na Dionis Nyato. 
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema kuwa ana ndoto kwamba siku moja sekta ya elimu itapewa kipaumbele cha kwanza nchini na kuzikomboa rasilimali za taifa la Tanzania zinazowanufaisha wageni na kuacha wananchi wakiambulia faida kidogo.Huku akimtaja Dk Martin Luther King aliyekuwa mwanaharakati wa haki za Wamarekani weusi aliyefariki kabla ya kuuona utimilifu wa ndoto yake, Lowassa alisema kuwa anamwomba Mungu asimwondoe duniani ili aweze kushiriki kuifanya ndoto hiyo kuwa kweli itakayokamilika siku si nyingi ambapo viongozi watakubali kuwa elimu bora ndiyo itakayowasaidia Watanzania kuchimba madini yao na kuyauza kwa faida duniani. 
Akizungumza wakati wa kuchangia SACCOS ya walimu ya Moshi Vijijini, Ushirika wa Stadium jana, Lowassa alisema kuwa katika ndoto yake anawaona viongozi wakikubali kwamba elimu bora ndiyo italisaidia taifa kuumiliki utalii na kunufaika nao, badala ya kuwaachia wageni wanufaike nao, huku Watanzania tukiambulia makombo.Wakati Lowassa akieleza ndoto yake hiyo, Mwenyekiti wa TLP na mbunge wa Vunjo Augustine Mrema amesema: “Biashara ya urais imenishinda namwachia Lowassa kwani mimi nimeamua kurudi kwenye biashara ya rejareja.”
“Ninayo ndoto kuwa siku si nyingi zijazo, elimu itapewa kipaumbele cha kwanza nchini Tanzania.Na namwomba Mwenyezi Mungu asiniondoe duniani, kabla sijauona utimilifu wa ndoto hii kama Dk King (Martin Luther) alivyoondolewa kabla hajaiona ndoto yake ikitimia, bali namwomba anipe muda na nguvu, niweze kushiriki katika kuifanya ndoto hiyo iwe kweli,” alisema Lowassa.Katika harambee hiyo ambapo zilipatikana jumla ya Sh1.3 bilioni , kati ya hizo fedha taslimu zilikuwa Sh250 milioni, Lowassa alifafanua kuwa itafika wakati ambapo elimu ya Tanzania itakuwa bora na kuwavutia majirani zake kuja kuwasomesha watoto wao nchini.Akizungumzia kudorora kwa elimu nchini, Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema kuwa bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya sekta ya elimu imekuwa ikitegemea fedha za wahisani kwa asilimia 70 na kwamba jambo la kusikitisha wahisani hao hawatoi fedha zote wanazoahidi, badala yake hutoa asilimia kati ya asilimia 40 na 50 ya fedha walizoahidi.“Bajeti yetu ya maendeleo ya sekta ya elimu kila mwaka haitekelezeki kwa upungufu wa asilimia 30-35. Kwa hali hii tutapataje maendeleo katika sekta ya elimu?” alihoji Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli mkoani Arusha na kuongeza: “Mwaka 1992 tulikuwa na Watanzania asilimia 15 tu wasiojua kusoma na kuandika, ilihali hivi sasa tuna Watanzania takribani asilimia 31 wasiojua kusoma.”Lowassa alisema kuwa wakaguzi wa shule za msingi na sekondari kushindwa kukagua shule zote nchini huchangia kushuka kwa elimu, akibainisha kwamba asilimia 20 pekee ya shule zote ndizo hukaguliwa kwa mwaka.
Alisema ili kufikia mafanikio yatakayoletwa na elimu, Serikali inapaswa kumjali mwalimu kwa kumpa motisha na mazingira mazuri ya kufundishia.
Akijibu hoja za watu wanaosema kuwa kuboresha huduma za walimu haiwezekani kutokana na idadi yao kuwa kubwa, alinukuu sehemu ya hotuba ya Rais wa zamani wa Marekani Franklin Roosevelt akisema: “ Kitu kimoja tunachopaswa kukiogopa ni woga wenyewe.”NA MWANANCHI

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...