Sunday, June 30, 2013

HUU NDIO WOSIA WA MZEE MANDELA NA MAHALI ANAPOPENDA KUZIKWA

Mzee Nelson Mandela ameandika wosia kwenye karatasi moja ya ukubwa wa A4 ambamo ameagiza azikwe katika milima iliyojitenga nyumbani kwa mababu zake huko Qunu, imebainika.

Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini, mwenye miaka 94, bado yuko mahututi lakini lakini hali yake inaimarika hospitalini mjini Pretoria ambako amekuwa huko kwa siku 21 zilizopita akitibiwa maambukizi kwenye mapafu.
Mnamo Januari 1996, wakati akiwa bado Rais, Mzee Mandela aliripotiwa kuandika wosia ambao aliagiza kufanyiwa maziko ya kawaida karibu na kijiji ambako alikulia kwenye rasi ya Mashariki.
Alisema kwamba wakati akifurahia kumbukumbu ya kulitumikia taifa hilo mjini Pretoria angetaka kuzikwa katika eneo la familia hiyo na kuwekewa jiwe la kawaida kama alama ya lilipo kaburi lake.
Gazeti la South African Mail na Guardian yaliripoti yakimnukuu rafiki wa siku nyingi wa familia akisema: "Hakuwahi kukifanya kifo kuwa jambo kubwa la kufikiriwa, lakini hakuwahi kutaka chochote cha ufahari".
Licha ya ukweli kwamba mauzo ya kitabu cha Mandela cha Long Walk To Freedom, na michoro yenye jina lake, kumpatia mamilioni ya pesa kwa hadhi wosia wake uliripotiwa kutosha kwenye karatasi moja ya ukubwa wa A4.
Kwa mujibu wa Shirika la utangazaji la Afrika Kusini SABC, swali hilo la sehemu atakayozikwa Mandela limeiudhi mno familia yake wiki hii.
Binti mkubwa wa Mandela, Makaziwe, na wanafamilia wengine 15 wameiomba mahakama imwamuru mjukuu wa Mandela kurejesha miili ya watoto watatu wa Mzee Mandela kwenye makaburi yao ya awali huko Qunu.
Mjukuu huyo, Mandla Mandela, anaaminika kuizika upya miili hiyo maili 13 kutoka hapo katika kijiji cha Mvezo, ambako anapanga kuanzisha madhabahu ya Mandela, hoteli na uwanja wa soka.
Mandla Mandela anatakiwa hadi leo awe amejibu madai hayo yaliyowasilishwa mahakamani, ripoti zilisema.
Nelson Mandela alijenga makazi yake baada ya kustaafu huko Qunu na alikuwa akiishi hapo hadi aliporejeshwa tena hospitali mara kwa mara hali iliyoanza mwishoni mwa mwaka jana.
Kiongozi huyo wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi alihudhuria mazishi ya mtoto wake wa kiume kwenye eneo la familia huko Qunu mwaka 2005, na ilitabiriwa kwa mapana kwamba kiongozi huyo mwenyewe atazikwa hapo.
Lakini mjukuu wake alihamisha miili ya watoto watatu wa Mandela na kuipeleka karibu na Mvezo, ambako ni sehemu aliyozaliwa rais huyo wa zamani na mjukuu huyo ana mamlaka kama Chifu.
Binti mkubwa Makaziwe na wanafamilia wengine wa Mandela wanataka miili hiyo ya familia kurejeshwa kwenye makaburi yao ya awali huko Qunu, kwa mujibu wa ripoti.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...