Sunday, June 30, 2013

JK AMGEUKA MWENYEKITI WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA JAJI JOSEPH WARIOBA

RAIS Jakaya Kikwete amemgeuka Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kwa kuridhia azimio la Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutaka uwepo muundo wa serikali mbili.
Rais Kikwete ambaye juzi aliongoza kikao cha Kamati Kuu (CC), mjini Dodoma, aliridhia azimio hilo, huku akijua fika kuwa ndiye aliyemruhusu Jaji Warioba kuingiza kipengele hicho kwenye rasimu wakati alipoifikisha mbele yake kabla ya kuitoa hadharani.
Kutoka na hali hiyo, Kamati Kuu imewataka wanachama wao wote kupitia mabaraza ya CCM kuhakikisha wanakubaliana na msimamo wa chama wa kupinga muundo wa serikali tatu kama ilivyopendekezwa na tume ya Jaji Warioba.
Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho kutoka Zanzibar, waliliambia Tanzania Daima Jumapili kuwa Kamati Kuu
imepitisha azimio la kutaka mabaraza ya Katiba ya chama hicho yajadili na kuridhia msimamo wa kuwa na serikali mbili.
Kamati Kuu ya CCM imekuja na mapendekezo ya namna ya kurekebisha kasoro kubwa za Muungano ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikilalamikiwa na Wazanzibari.
Vyanzo vyetu vya habari vilisema kuwa baadhi ya wajumbe wa CC kutoka Zanzibar walimshambulia Jaji Warioba kwa jinsi alivyoingiza suala la serikali tatu katika rasimu huku akiujua fika msimamo wa CCM.
Hata katika mkutano wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulhaman Kinana na wabunge wa chama hicho uliofanyika mjini Dodoma, umesisitiza suala la serikali mbili tu.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho kilichofanyika mjini Dodoma, zilisema kuwa wabunge nao walichambua kasoro nyingi za rasimu hiyo, kubwa kuhusu muundo wa muungano na mipaka yake.
“Kwenye mkutano wetu jana, tulikubaliana na msimamo wa Kamati Kuu wa serikali mbili na ndio ujumbe tunaupeleka kwa wananchi mikoani,” alisema mbunge mmoja alipozungumza na gazeti hili.
Mbali ya rasimu ya Katiba, Kamati Kuu ya CCM ilimshangaa Jaji Warioba kwa kupitisha sifa za wagombea urais na wabunge ambazo zinaweza kuleta mkanganyiko mkubwa siku za baadaye.
Katika mapendekezo ya rasimu kuhusu sifa za mtu kuwania ubunge, moja ya pendekezo hilo linasema kuwa, ikiwa “mtu huyo aliwahi kuwa mbunge kwa vipindi vitatu vya miaka mitano mfululizo, anapoteza sifa ya kuwa Mbunge.”
Katika sifa za kuwa rais, inasema, “ili uwe rais, lazima uwe na sifa za kuwa mbunge. “Hivyo kama umemaliza muda wa kuwa mbunge, maana yake hutakuwa na sifa za kuwania urais kwa vile huna sifa ya kuwa mbunge. Huu ni mkanganyiko mkubwa sana,” alisema mmoja wa wajumbe wa CC.
Zanzibar yataka iwe na Benki Kuu yake
Katika hatua nyingine, Baraza la Katiba Zanzibar (BAKAZA), limekuja na mapendekezo mapya kuhusu rasimu mpya ya Katiba ya Muungano.
Katika mapendekezo hayo, BAKAZA limetaka Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa kuondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano.
Mapendekezo hayo yametolewa na Mwenyekiti wa BAKAZA, Profesa Abdul Sheriff katika mkutano wake na vyombo vya habari.
Mapendekezo mengine ni kutaka Benki Kuu (BoT), vyama vya siasa na uhamiaji yaondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano, pamoja na rasimu hiyo mpya kuzingatia utaratibu wa Rais wa Jamuhuri ya muungano kupatikana kwa zamu kati ya washirika wa pande mbili za Muungano wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Profesha Sheriff alisema mapendekezo hayo yametokana na uchambuzi wa rasimu ya Katiba ya Muungano wa Tanzania iliyotolewa Juni 3, mwaka huu.
Alisema hakuna sababu ya maana ya Polisi na Usalama wa Taifa kuendelea kubaki katika orodha ya mambo ya Muungano katika mfumo wa serikali tatu.
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo imeelezwa kuwa Ibara ya 217 ya rasimu ya Katiba ifutwe na kuruhusu kila mshirika wa Muungano kuwa na Benki Kuu yake itakayokuwa na mamlaka ya kusimamia sera za fedha pamoja na kuangalia mwenendo wa uchumi wa nchi husika, Tanganyika na Zanzibar.
“Ni vema Zanzibar ikawa na mfumo wa sarafu yake na Benki Kuu yake ili iweze kudhibiti na kuendesha uchumi wake bila ya kuathirika na Muungano kama ilivyo kwa Hong Kong na Macau ndani ya Jamhuri ya Watu wa China,” alisema.
Hata hivyo BAKAZA imesema kuwa kama suala la Mambo ya Nje litaendelea kubakia katika orodha ya mambo ya Muungano, basi nafasi za watendaji na mabalozi zitolewe kwa usawa Zanzibar.
Mapendekezo hayo ambayo yanafungamana kwa kiwango kikubwa na msimamo wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, Ibara ya 2 ya rasimu ya Katiba wametaka kuingizwa haki ya nchi mshirika wa Muungano kujitoa kwa kutumia utaratibu wa kura ya maoni, kama ataona hakuna manufaa yoyote katika muungano huo.
Profesa Sheriff aliwaambia waandishi wa habari kuwa muhtasari wa mapendekezo hayo ndio utakuwa muongozo mkuu wakati wa kutoa elimu kwa wajumbe wa mabaraza ya Katiba katika visiwa vya Unguja na Pemba.

TANZANIA DAIMA

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...