Siku
moja baada ya shirikisho la soka nchini TFF kubadilisha ratiba ya
baadhi ya mechi za ligi kuu ya Tanzania bara ili kuweza kufanikisha
mpango wa kuonyesha mechi hizo kupitia kituo cha Supersport, klabu ya
Yanga kupitia makamu wake mwenyekiti Clement Sanga imesema haikubaliani
na mpango huo kwasababu haujafuata utaratibu na pia utaziingizia hasara
kubwa klabu zinazohusika na mpango huo.
"Kwanza
jambo muhimu kuhusu suala hili kumekuwepo na mfumo m'bovu wa
mawasiliano baina ya TFF, Supersport na vilabu vyenyewe kama Yanga.
Sisi kwa upande wetu tunaona kabisa huu mpango unatuingizia hasara sana,
kwa mfano baada ya kubadilisha ratiba ya mechi zetu tutacheza mechi 3
ndani ya siku 8 wakati ilitakiwa ndani ya wiki tucheze mechi mbili na
bado ukumbuke bado tunapaswa kusafiri kwenda Tanga hivyo kuna mambo ya
gaharama na vitu vingine vingi tu. Lakini pia mechi ambazo wanataka
kuzionyesha bure ni zile ambazo sie vilabu tunazitegemea sana kwenye
suala zima la mapato na wao ndio wanataka kuzionyesha bure - na
watanzania wengi wanaposikia hivyo mahudhurio uwanjani yanakuwa hafifu
hivyo tunakosa mapato. Bora waonyeshaji wa mechi hizo wangekuwa wanatoa
fidia kiasi fulani kutokana na matangazo ya kibiashara wanayopata ili
kuweza kuzinufaisha klabu zetu, lakini si hivyo wanavyotaka wao. Nadhani
kwenye hili TFF wangeliangalia vizuri liweze kutunufaisha sote na sio
watu wachache kama ilivyo sasa," Aliongeza Sanga.
Alipoulizwa
kama wameshawasilisha msimamo wao kwa uongozi wa TFF na kamati ya ligi
Clement Sanga alisema, "Kwanza walipotuletea taarifa kuhusu jambo hilo
kwa njia ya barua pepe tuliwajibu na baadae ikaja barua ambayo katibu
wetu alijibu kutoa msimamo wetu juu ya suala hili, kinachojitokeza hapa
TFF wanatumia mabavu yao kutupeleka peleka, sie tumeshika makali wao
mpini. Sie tusipokubali kucheza jumatano kama wanavyotaka wao basi
watachukua maamuzi ya kuigawia timu pinzani ushindi, la msingi sie
tutakalolifanya hatutokubali mechi zetu zionyeshwe kwenye TV bila
kupata fidia ya fedha. Sisi kama Yanga hatupo tayari kuona tunafanyishwa
kazi bure. Supersport imeshafanya majaribio sana, sasa haya ya sasa
nini? Viongozi wa soka tubadilike tuweke mbele maslahi ya soka letu
kabla ya kujiridhisha nafasi zetu, haiwezekani watu wawili watatu
waamue tu kwamba mechi kesho hakuna bila kujali hasara
zitakazowagharimu wengine. Sie tulishajipanga kwamba Jumatano tunacheza
na Oljoro, then tunasafiri kwenda Tanga kucheza na Mgambo then turudi
Dar kwa ajili ya mchezo mwingine. Matayarisho ya mechi hizi tulishafanya
wiki mbili kabla, tukalipia hotel na gharama nyingine, sasa
haiwezekani ghafla kikundi cha watu fulani wenye nguvu za kimaamuzi
kutubadilishia ratiba - je zile fedha tulizolipa mahoteli
watatulipaakina nani, kwa sababu ni dhahiri unapolipia hotel unapewa na
muda wa kuivitumia vyumba vile hivyo muda ule unapoisha fedha yako
inakuwa imeenda. Nadhani hili suala linahitaji kuangaliwa vizuri, na
viongozi wa vilabu tuwe na umoja kuweza kulipigania hili suala dhidi
yetu. Tusiwe viongozi wa kuburuzwa ovyo ovyo."
Akizungumzia
mahitaji wanayotaka ili wakubali mechi zao ziweze kuonyeshwa kwenye
TV, Sanga alisema kwamba hicho kituo cha TV kinachotaka kurusha
matangazo ya moja kwa moja ya mechi zao inabidi walete ofa ya kueleweka
ambayo itaweza kufidia hasara ya kwenye mapato na gharama nyingine
ambazo timu wataziingia ili kuweza kwenda sawa na ratiba zao. Pia
akataka uwepo uwazi wa makubaliano yote ya kimsingi ili kuepusha
migogoro ya namna hii.
No comments:
Post a Comment