Wananchi wa Zimbabwe leo wanapiga kura ya maoni kuhusu katiba mpya ambayo itaweka kikomo cha muhula wa urais na kuongeza uhuru wa vyombo vya habari. 
Hata hivyo, wasiwasi umeongezeka baada ya wanachama kadhaa wa chama cha upinzani cha Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai kushambuliwa wakati wakifanya kampeni katika kitongoji cha Mbare kwenye mji mkuu Harare, hapo jana.
Msemaji wa chama hicho cha Movement for Democratic Change-MDC, Douglas Mwonzora, amewashutumu wafuasi wa Rais Robert Mugabe kuhusika na tukio hilo.
Katiba hiyo mpya itadhibiti mamlaka ya Rais Mugabe na kuweka misingi ya kufanyika kwa uchaguzi mwezi Julai, mwaka huu.
Uchaguzi huo utahitimisha makubaliano yaliyokumbwa na matatizo ya kugawana madaraka kati ya Rais Mugabe na Waziri Mkuu Tsvangirai.-DW.