Monday, March 25, 2013

UKWELI KUHUSU ELIMU YA NAIBU WAZIRI WA MH. MLUGO HUU HAPA



Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo anadaiwa kutumia ujanja katika wasifu na elimu yake ambapo katika maisha yake ya kielimu ametumia majina manne tofauti.
Philipo Augustine Mulugo ndiyo jina lake halisi ambalo alilisomea mpaka alipohitimu darasa la saba kwa mara ya kwanza 1988, lakini kutokana na kwamba hakufaulu kwenda sekondari alirudia darasa hilo.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa takriban miezi mitatu sasa umebaini kuwa 1989, Mulugo alirudia darasa la saba katika Shule ya Msingi Rukwa ya mkoani Mbeya akitumia jina la Hamimu Hassan.

Imebainika kuwa kabla ya kuhitimu darasa la saba kwa mara ya pili, alibadili jina hilo (kutoka Hamimu Hassan) na kuwa Hamimu Augustino ambalo aliendelea nalo wakati akisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari kutwa ya Mbeya (Mbeya Day) mwaka 1990.

Hata hivyo, Mulugo mwenyewe akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam alipuuza tuhuma hizo kwa kusema kuwa ni njama za kisiasa zinazofanywa na maadui zake. Mulugo anasema madai hayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na amekuwa akiyajibu kwa kuwaonyesha vyeti vyake halali vya shule.

“Hayo madai ni ya muda mrefu, wewe sijui utakuwa mtu wa 20 kuuliza swali kama hilo. Mimi vyeti ninavyo na hata ukitaka ushahidi nitakuonyesha,” alisema Waziri Mulugo na kuongeza:

“Haya mambo kabla hata sijachaguliwa kuwa Mbunge, tulivyokuwa bado kwenye mchujo wa ndani, usiku wa manane watu walisambaza huu uvumi na nilivyoenda kwenye kikao nikatoa vyeti vyangu, wakaviona.”

Waliomfundisha

Baadhi ya walimu waliomfundisha Mulugo, watu waliofanya kazi naye pamoja na wakazi wa Kijiji cha Udinde alikozaliwa, maelezo yao yanathibitisha mabadiliko ya majina ya Mulugo kwa nyakati tofauti pia ngazi mbalimbali za kielimu.

Uchunguzi unabainisha kuwa baada ya kuhitimu kidato cha nne, alifaulu kwenda Shule ya Sekondari ya Wavulana, Songea ambako alisoma kati ya 1994 na 1996 akiendelea kutumia jina la Hamimu Mulugo.

Baada ya kuhitimu kidato cha sita, uchunguzi ulibaini kuwa Mulugo alirejea Mbeya na 1998 alilazimika kubadili tena jina pale alipotumia cheti cha mtu aitwaye Dickson Mulungu, kuombea kazi ya kufundisha katika Shule ya Sekondari ya Southern Highlands.

Habari zinasema Mulugo alichukua hatua hiyo ili kumshawishi mmiliki wa shule hiyo mfanyabiashara, Gulnoor Dossa (sasa ni marehemu), kumpa nafasi ya kufundisha shuleni hapo.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...