*Usafiri wa helikopta waitafuna dola mara 71 ya gharama ya gari
ULINZI wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, akiwa gerezani na anapopelekwa mahakamani, umeanza kuvitesa vyombo vya Dola. Habari zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na Kamanda wa Kikosi cha Anga wa Jeshi la Polisi, zinaeleza kuwa serikali juzi ilitumia kiasi cha shilingi 10,682,031 kama gharama za usafiri wa helikopta za kumpeleka na kumrudisha kiongozi huyo mahakamani mkoani Morogoro.
MTANZANIA Jumatano kupitia vyanzo vyake vilivyoko ndani na nje ya Jeshi la Polisi, limedokezwa kuwa gharama za kurusha helikopta kwa dakika 45 hadi saa moja ni dola za Marekani 3,000 hadi 3,300 ambazo ni sawa na shilingi 5,341,032.85 .
Hivyo gharama za kwenda na kurudi kwa saa jumla yake ni dola za Marekani 6,600 ambazo ni sawa na shilingi 10,682,031.
Akithibitisha hilo, Kamanda wa Kikosi cha Anga wa Jeshi la Polisi, Antony Mwami alisema gharama za kurusha helikopta kwa dakika 45 ni dola 3,000 ambazo ni sawa na shilingi milioni tano.