Kwa maneno ya siku hizi ni
kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema
'amelikoroga na kulinywa mwenyewe', baada ya jana kutoa kauli ya kuudhi
alipomtaka mbunge kutoka Zanzibar akaulize swali lake visiwani humo,
iliyosababisha baadhi ya wabunge kususia Bunge na kutoka.
Kauli iliyoonyesha kuwagawa wabunge
katika mafungu mawili; wa bara na Zanzibar, ilimlazimu Jaji Werema
baadaye kusimama bungeni na kuwaangukia akiwaomba radhi waliokerwa na
kauli yake na pia kuliomba radhi Bunge, Spika wake, Anne Makinda na
wananchi.
Kuondoka kwa wabunge hao kulitokana na
mwongozo wa Spika ulioombwa na Mbunge wa Ole (CUF), Rajabu Mbarouk
Mohamed kutokana na majibu Jaji Werema kwa mbunge wa Mkanyageni (CUF),
Habibu Mnyaa aliyekuwa ameomba ufafanuzi wakati Bunge lilipokaa kama
kamati ya kupitisha vifungu vya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2014/15. Mnyaa alisema Wizara ya Katiba na
Sheria ni muhimu lakini imekuwa ndiyo ya kwanza kuvunja sheria na haki
za binadamu na akataka ufafanuzi.
Hata hivyo, aliposimama kujibu swali
hilo, Jaji Werema alimwambia Mnyaa kuwa mambo mengine akaulize Zanzibar
na siyo katika Bunge la Jamhuri kwa kuwa si kila kitu kitaulizwa ndani
ya Bunge hilo. "Alichokizungumza Mnyaa ni sahihi
lakini hapa si mahali pake, namshauri kuwa akaulize huko Zanzibar kwenye
vikao vyao hapa sisi hatuna majibu," alisema Werema. Tafadhari Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz