Maelfu ya watu nchini Israel wamekuwa wakitoa heshima zao za mwisho kwa hayati Ariel Sharon kabla ya mazishi yake hii leo.
Jeneza la Sharon liliwekwa nje ya
majengo ya bunge mjini Jerusalem jana Jumapili huku waombolezaji
wakimiminika kumtolea heshima za mwisho kabla ya maziko. Sharon alifariki akiwa na umri wa miaka 85 baada ya kuwa hali mahututi kwa miaka 8, akitumia mashine kupumua. Atafanyiwa ibada maalum ya kitaifa leo kabla ya kuzikwa karibu na shamba lake eneo la Sderot.
Waisreli pamoja na viongozi wa dunia,
wametoa heshima zao za mwisho , lakini wale ambao wanaweza kusema
hawajaguswa sana na kifo cha Sharon ni wapalestina. Mwili wa Sharon ulifikishwa katika bunge la taifa Jumapili ambapo watu waliruhusiwa kuutizama siku nzima. Maombi yalifanywa huku bendera zikipepea nusu mlingoti. Watu waliendelea kumiminika nje ya jengo hilo wengine wakiwasha mishumaa katika hatua ya kumuenzi Sharon.
Wageni mashuhuri wanatarajiwa
kuhudhuria ibada maalum ya Ariel katika bunge la taifa wakiwemo makamu
wa Rais wa Marekani Joe Biden, waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei
Lavrov, mjumbe maalum wa Mashariki ya kati Tony Blair, na waziri wa
mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier.
Sharon anakumbukwa na wengi kwa siasa
zake na harakati zake dhidi ya wapalestina wakati akiwa mwanajeshi.
Aliidhinisha ujenzi wa makazi ya walowezi katika eneo la Palestina na
pia baadaye tume ya uchunguzi ilimpata na hatia ya kukosa kuzuia mauaji
ya wapalestina yaliyofanywa na wakristo wa Phalangist baada ya Iisrael
kuvamia Lebanon.
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz