Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kitamshitaki Balozi wa China nchini, Lu Younqing Umoja wa Mataifa (UN) kwa kukiuka Mkataba wa Vienna (Vienna Convention) wa mwaka 1964 ambao unaeleza uhusiano wa kibalozi kati ya nchi na nchi.
Aidha, kimesema kitaiandikia barua Serikali ya
China ili kutaka ufafanuzi kama imemtuma Balozi wake kufanya kazi ya
uenezi siasa kwenye vyama.
Tukio la Balozi huyo kuhudhuria mkutano wa hadhara
wa CCM lilitokea Septemba tisa mwaka huu kwenye mkutano wa chama hicho
uliofanyika Wilaya ya Kishapu Shinyanga, ambapo Katibu Mkuu wake,
Abdulrahman Kinana alimtambushisha balozi huyo huku akiwa amevaa sare za
chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam
jana, Waziri kivuli wa mambo ya nje ambaye pia ni Mbunge wa Nyamagana
Jijini Mwanza, Ezekiel Wenje alisema Chadema wameamua kuchukua hatua
hizo ili kukomesha vyama vya siasa kutumia mabalozi kama wawakilishi wa
vyama vyao kwa kufanya uenezi kwenye mikutano ya siasa.