Mfanyabiashara maarufu nchini, Alex Massawe amefikishwa
mahakamani Dubai, Falme za Kiarabu (UAE), kwa tuhuma za mauaji baada ya Serikali
ya Tanzania kupitia Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol), kuiomba Serikali
ya nchi hiyo kumkamata.
Massawe anayetarajiwa kuletwa nchini wakati wowote
kuanzia sasa, alikuwa anatafutwa na Polisi wa Tanzania kwa muda mrefu na
alikamatwa Dubai, mapema Julai na maofisa wa usalama wa UAE baada ya alama zake
za vidole kuonyesha kuwa alikuwamo kwenye orodha ya watu waliokuwa wanasakwa na
Interpol.
Baada ya kukamatwa, Mkuu wa Interpol, Tawi la Tanzania,
Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile alisema Massawe alikamatwa kati
ya Juni 20 na 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai
akitokea Afrika Kusini.
Massawe ambaye anafanya biashara zake katika Miji ya
Arusha, Dar es Salaam na Moshi, inadaiwa kwamba akiwa Dubai, alikutwa na pasi
tatu bandia za kusafiria zilizokuwa na majina tofauti wakati alama zake za
vidole zilionyesha anaitwa Alex Massawe. “Ombi la kuleta mhalifu nchini kutoka
nje ya nchi (extradition request), lina hatua ndefu.
Unajua kuna mlolongo wa taratibu za kutekeleza. Kwanza lazima Polisi wa Tanzania watoe tangazo kwa Interpol kuhusu kumsaka mtu huyo ili aletwe,” alisema Babile.
Unajua kuna mlolongo wa taratibu za kutekeleza. Kwanza lazima Polisi wa Tanzania watoe tangazo kwa Interpol kuhusu kumsaka mtu huyo ili aletwe,” alisema Babile.