WAMO DEWJI,
LWAKATARE, RUTABANZIBWA
WABUNGE Mohamed Dewji wa Singida mjini na
Mchungaji Getrude Lwakatare wote wa CCM pamoja na mfanyabiashara maarufu jijini
Dar es Salaam Robery Mugishagwe wametajwa kuwa vinara wa uvamizi na uuzaji wa
viwanja jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa, naye ametajwa kumkingia kifua mmoja
wa wavamizi wa viwanja kwa kumuwekea dhamana alipofikishwa polisi.
Waziri wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais,
Dk. Tereza Huviza ndiye aliyewataja vigogo hao jana jijini Dar es Salaam,
alipokuwa akizungumza na wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Maliasili,
Ardhi na Mazingira, iliyokwenda kutembelea ofisi za Baraza la Mazingira
(NEMC).
Huvisa alikuwa akihofia kutaja majina ya vigogo
hao, lakini Mwenyekiti wa kamati hiyo, James Lembeli, alimkasirikia na kumhoji
ni nani hapa nchini aliye juu ya sheria kiasi cha kumfanya aogope kumtaja licha
ya kuvunja sheria.
Lembeli alimtaka Waziri Huvisa kuyataja majina
hayo kwani akiendelea kuwahofia watu wa aina hiyo, wataendelea na uvamizi huo na
watakapofika 100 wenye tabia hizo nchi haitatawalika.
“Huna sababu ya kuogopa kuwataja watu waovu,
kamati hii ina mamlaka kisheria…usihofie chochote, wataje tujue namna ya
kuwashughulikia,” alisema Lembeli.
Shinikizo hilo la Lembeli liliungwa mkono na
wajumbe wote wa kamati hiyo waliomuhakikishia usalama Waziri Huvisa aliyeonekana
kuwa na hofu wakati akiulizwa maswali.
Baada ya kuhakikishiwa usalama, alianza kumtaja
Dewji ambaye alisema anashinikiza kupewa eneo la ufukwe karibu na zilipo ofisi
za ubalozi wa Urusi hapa nchini huku akijua ni kinyume cha sheria.