HOFU YAKIMBIZA
WAPIGA KURA
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeibuka na ushindi mnono katika uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata nne za jijini Arusha.
Katika Kata ya Elerai, mgombea wa CHADEMA
Injinia Jeremia Mpinga alimbwaga Emanueli Laizer wa CCM kwa kura 1,715, dhidi ya
1,239.
Kata hiyo ilikuwa na wapiga kura 23,797
waliojiandikisha na vituo 55 vya kupigia kura, lakini idadi kubwa ya wananchi
hawakujitokeza.
Matokeo ya kura yalitangazwa chini ya ulinzi
mkali wa askari polisi zaidi ya 40 wenye silaha, na kupokelewa kwa shangwe kubwa
na wafuasi na mashabiki wa CHADEMA.
Katika Kata ya Kaloleni, mgombea wa CHADEMA,
Kessy Emmanuel Miliare alimshinda kwa mbali mgombea wa CCM kwa kura 1,470 dhidi
ya 530, wakati mgombea wa CUF ameambulia kura 275. waliojiandikisha 12,674
waliopiga kura 2,292. Kura halali ni 2,277 na zilizoharibika 15.
Akitangaza matokeo katika Kata ya Themi,
Msimamizi wa Uchaguzi, Editha Mboye alimtangaza mgombea udiwani wa CHADEMA,
Mallance Kinabo kuwa mshindi kwa kupata kura 678, akimwacha mbali mgombea wa CCM
Victor Mkolwe aliyepata kura 326, huku yule wa CUF, Lebora Ndervai akipata kura
313.
Kata ya Kimandolu, CHADEMA pia wameibuka na
ushindi mkubwa na kuiacha vibaya CCM.
Mgombea wa CHADEMA, Elishadai Ngowi amemshinda
mgombea wa CCM, Edina Sauli kwa kura 2,265, dhidi ya 1,169 za mpinzani
wake.